2015-05-27 11:04:00

Uchumba ni shule ya upendo, imani, matumaini na wajibu wa kujenga familia


Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mwendelezo wa Katekesi yake kuhusu Injili ya Familia, Jumatano, tarehe 27 Mei 2015 amejikita katika mchakato wa uchumba unaohitaji kujenga na kuimarisha imani, uaminifu na matumaini kwa kutambua kwamba, ndoa ni wito mtakatifu kutoka kwa Mwenyezi Mungu unaosimikwa katika upendo thabiti. Uchumba ni kipindi cha wanandoa watarajiwa kufahamiana kwa undani zaidi, tayari kujenga na kudumisha msingi wa Familia kama Kanisa dogo la nyumbani.

Baba Mtakatifu anasema, upendo ni fadhila ambayo inahitaji kwa namna ya pekee kabisa maandalizi, yanayowawezesha wanandoa watarajiwa kuwa huru, wakarimu na makini katika maamuzi yao yatakayowasaidia kudumu katika agano la upendo kwa maisha yao yote. Kutokana na umuhimu huu, Kanisa linapenda kukazia kwa namna ya pekee kipindi cha uchumba kwa kutoa semina mbali mbali ili kuwaandaa wanandoa watarajiwa kutekeleza dhamana na majukumu yao barabara.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, kwa njia ya ushuhuda wa mifano na msaada wa wanandoa wa Wakristo, wanandoa watarajiwa wanahamasishwa kufanya tafakari ya kina kwa pamoja kuhusiana na upendo wao, maisha yao kwa siku za usoni pamoja na kuangalia umuhimu wa fadhila ya imani na maisha ya sala wanayotarajiwa kushirikishana kama mke na mme.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuwaombea wanandoa watarajiwa, ili waweze kujiandaa kikamilifu katika siku yao ya ndoa kwa hekima, busara, imani na matumaini yanayobubujika kutoka katika Kristo Yesu na kamwe wasimezwe na malimwengu wala kubeza siku hii muhimu katika maisha yao. Baba Mtakatifu anazitakia familia zote furaha na amani katika Kristo.

Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa vyama vya utume wa familia kutoka sehemu mbali mbali za dunia; vijana wanaojiandaa kwa ajili ya kupokea Sakramenti ya Kipaimara na Ekaristi Takatifu; wote hawa waweze kujaliwa kumpokea Roho Mtakatifu atakayewawezesha kuwa kweli ni mashuhuda na watangazaji wa Injili ya Furaha na upendo wa Kristo. Watu watambue kwamba, maisha ni zawadi ya thamani kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu.

Waamini waendelee kumwomba Bikira Maria ili awasaidie kuwa kweli ni alama ya imani na matumaini kwa ndugu na jirani zao; daima wajitahidi kuwa na amani na utulivu katika familia zao. Kipindi cha uchumba ni shule ya upendo na uwajibikaji, kiroho na kimwili, kwa ajili ya kukumbatia mchakato wa uundaji wa familia mpya.

Baba Mtakatifu pamoja na kutambua uwepo wa makundi ya mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia, lakini kwa namna ya pekee kabisa amewataja washiriki wa mkutano wa Mfuko wa “Centesimu Annus” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro ambao kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 27 Mei 2015 wamekuwa wakifanya mkutano wao hapa mjini Vatican na kuwashirikisha viongozi wakuu waandamizi kutoka Vatican. Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini kwamba, Kanisa linaendelea kuadhimisha kumbu kumbu ya Jubilei ya miaka mia tano tangu alipozaliwa Mtakatifu Filippo Neri. Ni Kiongozi wa Kanisa aliyeanzisha vituo vya michezo kwa vijana, akashuhudia furaha, imani na matumaini yaliyokuwa yanabubujika kutoka kwa Kristo, changamoto na mwaliko kwa vijana kuiga mfano wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.