2015-05-27 11:53:00

Kanisa linamkumbuka Hayati Kardinali Bernadin Gantin, Baba na Mchungaji


Mama Kanisa anafanya kumbu kumbu ya miaka saba tangu Kardinali Bernardin Gantin, kutoka Benin, alipofariki dunia. Alikuwa ni Padre na mchungaji mahiri aliyejitosa kimasomaso kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu tangu akiwa bado kijana, akawa ni kielelezo na utambulisho wa Kanisa Barani Afrika. Hivi karibuni, mjini Roma kumefanyika hafla fupi kwa ajili ya kumkumbuka Kardinali Gantin, tukio ambalo limehudhuriwa na Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali.

Wengine waliohudhuria ni pamoja na Kardinali Francis Arinze, Robert Sarah, Bwana Thèodore C. Loko, Balozi wa Benin mjini Vatican pamoja na Bwana Jean-Claude Michel, Dekano wa Mabalozi wanaowakilisha nchi na mashirika ya kimataifa mjini Vatican. Kardinali Gantin anakumbukwa kwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Baadaye akateuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu; Baraza la Kipapa la haki na amani; Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum na Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maaskofu. Leo hii watu wamezoea kuona nyuso za viongozi kutoka Barani Afrika wakishika nyadhifa mbali mbali katika Kanisa la kiulimwengu, lakini ikumbukwe kwamba, Kardinali Bernadin Gantin alikuwa ni Kardinali wa kwanza kutoka Barani Afrika aliyepewa dhamana ya kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa.

Katika tukio hili Kardinali Angelo Sodano akirejea kwenye Maandiko Matakatifu anasema kwamba, “wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia Neno la Mungu; tena kwa kuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao”. Kardinali Sodano amemkumbuka Hayati Kardinali Gantin ambaye katika ujana wake, alipewa dhamana ya kuliongoza, Jimbo kuu la Cotonou, nchini Benin hapa akaonesha sifa za mchungaji mwema kati ya watu wake na kuwa rejea katika mchakato wa maisha ya kiroho kabla ya kuhamishiwa mjini Vatican ili kuendelea na utume kwa ajili ya Kanisa la Kiulimwengu.

Balozi Jean-Claude Michel anamkumbuka Kardinali Gantin kuwa ni kiongozi aliyejisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa. Alibahatika kuwa na karama ambazo alizifanyia kazi kwa umakini mkubwa. Alikuwa ni kiongozi mwema, mkarimu, mnyenyekevu na mtu mwenye upendo; tunu ambazo aliwashirikisha wale wote waliobahatika kukutana naye katika maisha na utume wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.