2015-05-26 14:47:00

Watawa wanachangamotishwa kuwa ni vyombo vya huruma, upatanisho na amani


Mkutano mkuu wa Shirika la Ndugu wadogo, imekuwa ni fursa ya kutafakari na kusali kwa kuongozwa na mambo msingi katika maisha ya kitawa na kwa namna ya pekee wameangalia utambulisho wao kama ndugu wadogo na umuhimu wa udugu. Huu ni mwaliko kwa watawa hawa kujisikia wadogo mbele ya Mwenyezi Mungu ili kukimbilia na kukumbatia huruma yake isiyokuwa na mipaka, ili kuwamegea wale ambao ni wadogo zaidi, yaani: maskini na wadhambi mbele ya Mungu, ili kuweza kukaribia na hatimaye kupata wokovu.

Katika Maandiko Matakatifu wale ambao walijitambua kuwa ni wadogo mbele ya Yesu waliweza kuokolewa, lakini wale waliodhani kwamba, hawana haja na wokovu walijikwaa. Udogo ni dhana inayomwezesha mtawa kutoka katika ubinafsi wake na hivyo kuvukwa mipaka ya miundo mbinu iliyowekwa, muhimu sana ikiwa kama itatumika barabara.

Ni changamoto ya kuondokana na mazoea na usalama, tayari kushuhudia uwepo wa watawa karibu na maskini, wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kuwashirikisha upendo na huruma ya Mungu kwa njia ya huduma makini. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne tarehe 26 Mei 2015 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wanaoshiriki katika mkutano mkuu wa Shirika la Ndugu wadogo.

Anasema, dhana ya udugu ni muhimu sana katika ushuhuda wa Kiinjili kama inavyojionesha kwa Wakristo wa Kanisa la mwanzo waliojitahidi kujenga msingi wa Kanisa katika umoja na upendo; wakawashangaza wengi kwa toba, msamaha na huruma walionjeshana katika hija ya maisha yao wakati wa raha, shida na uzoefu wa maisha. Hii ndiyo changamoto ambayo Shirika la Ndugu wadogo linahamaishwa kuimwilisha ili kujenga imani katika mahusiano kati ya watu, ili watu waweze kuona na kuamini kwa kutambua kwamba, upendo wa Kristo unaponya madonda na kuwaunganisha ili kuwa kitu kimoja.

Watambue kwamba, wao ni vyombo vya huruma, upatanisho na amani; mambo msingi yanayotekelezwa mintarafu wito na utume wao, daima wakijitahidi kutoka ili kwenda kuhubiri mintarafu karama ya Shirika linalotumwa kwenda ulimwenguni kote, huku wakiwajibishwa na upendo wa Kristo kama anavyowaalika Mtakatifu Francisko. Huko wasigombane wala kuhukumiana; bali wajitahidi kuwa watu wema, wenye amani, watu wenye kiasi, wanyenyekevu na wakweli, huku wakiendelea kugawa amani. Hiki ni kielelezo cha unabii na udugu hata katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu anawataka watawa kujenga utamaduni wa majadiliano, amani na utulivu na watu wote, kwa kujikita katika ufukara, kwa kuwatangazia watu amani pamoja na kuridhika na maisha yao ya kitawa. Wawe wakweli na wawazi; watumiaji wazuri wa mali ya Shirika kwa kuzingatia kanuni maadili na mshikamano pamoja na kujikana. Kamwe watawa wasikite maisha na usalama wao katika mali ya dunia, bali wawe kweli ni mashuhuda wa udogo na ufukara ambao kwa njia ya Mtakatifu Francisko wa Assis wanaalikwa kuumwilisha. Baba Mtakatifu anawaonya kwamba, wasipokuwa ndugu wadogo wanaojikita katika ufukara, wanaweza kuumbuliwa na walimwengu.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawakumbusha watawa kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu ambaye ni mhamasishaji mkuu wa  mahusiano na utume wao katika Kanisa, ili aweze kuwaongoza kugundua neema na siri ya udugu wao chachu ya huduma kwa jirani na alama wazi ya uwepo wao ndani ya Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake.

Mwanga wa Roho Mtakatifu utawawezesha kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuliwa katika ulimwengu mamboleo, kutokana na kupungua kwa idadi ya watawa, ongezeko la wazee na idadi ndogo ya vijana wanaokumbatia miito mipya. Mwishoni, Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime katika hija ya maisha na utume wao kwa kutambua kwamba, kuna watu wengi wanaofurahishwa na utume wao kama wafanyavyo pia viongozi wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.