2015-05-26 08:36:00

Mahojiano kati ya Gazeti la "La Voz del Pueblo" na Papa Francisko!


Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni amefanya mahojiano maalum na Gazeti la “Voz del Pueblo” linalochapishwa nchini Argentina, kwa kuelezea vipaumbele katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa namna ya pekee anabainisha mahusiano yake na watu anaokutana nao katika hija ya maisha na utume wake, jinsi ambayo anautumia muda wake katika kutekeleza majukumu mbali mbali; matumaini na wasi wasi ambao uko moyoni mwake. Amemwambia mwandishi wa habari Juan Berreta kwamba, katika maisha yake alipenda sana kutembea na kufurahia maisha ya kawaida ya watu wa mtaani; haya ni kati ya mambo ambayo kwa sasa anayakosa kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu anasema, daima anawaomba waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala kwani anatambua kwamba, sala za watu zinamwimarisha katika maisha na utume wake. Hii ni kiu ya maisha ya roho. Anasema katika maisha yake hakuwahi hata siku moja kuota kwamba, angeweza kuchaguliwa kuliongoza Kanisa. Baadhi ya waandishi wa habari kutoka Uingereza walikuwa wamempatia nafasi ya arobaini na sita, kati ya Makardinali ambao walidhani kwamba, wangefaa kuliongoza Kanisa.

Baada ya kuchaguliwa, akaendelea na maisha yake kama: mtawa na Myesuiti, akajiweka chini ya ulinzi wa Mwenyezi Mungu na kwamba, wakati wa kuhesabu kura, muda ulionekana kana kwamba, umesimama, lakini aliendelea kusali Rozari kwa moyo wa utulivu. Anasema, anapokuwa kati ya watu kwa ajili ya watu anajisikia vyema zaidi na wala hadi sasa hajui siri ya mvuto huu na anadhani kwamba, watu wanajitahidi kufahamu kile ambacho anataka kuwashirikisha kutoka katika undani wa maisha yake. Anapenda kuyakita maisha yake kwa ajili ya watu na kwamba, hawezi kuishi bila ya kukutana na kuzungumza na watu, vinginevyo atateseka sana moyoni mwake.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, yataka moyo kweli kweli! Zamani alipokuwa Kardinali alikuwa ni mtu huru, alikuwa anatembea na kula Pizza kadiri ya hamu yake. Ni kweli kabisa kwamba, anaweza kuomba Pizza iletwe Vatican, lakini utamu wake unapungua kwa kiasi fulani! Alikuwa ni mtembezi na alipenda kutumia vyombo vya usafiri vya umma kama watu wengine wa kawaida. Anakiri kwamba, yeye ni mtu ambaye hapendi sana kuzingatia itifaki, lakini kwa masuala rasmi anajitahidi kufuata maelekezo.

Baba Mtakatifu anasema, anapata usingizi wa kutosha na kadiri ya ratiba yake anaamka kila siku  majira ya saa 10: 00 asubuhi. Kila siku anajipatia muda walau wa saa moja kujisomea na anaamka mwenyewe na kwamba, anaheshimu sana muda wa mapumziko mara baada ya chakula. Siku ambayo anakosa “Siesta” Baba Mtakatifu anasema, inamtendea sana.

Baba Mtakatifu anasema kilio na machozi yake ni kwa ajili ya shida na mahangaiko ya watu mbali mbali; wahamiaji na wakimbizi; watoto wagonjwa pamoja na wafungwa. Anasema kuna watu wengi wanafanya makosa lakini bado hawajahi kukamatwa na kufungwa gerezani. Anawalilia kwa uchungu Wakristo wanaoendelea kuuwawa, kuteswa, kunyanyaswa na kudhulumiwa kikatili.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, katika maisha yake hana kitu ambacho kinamwogofya kwani amejikabidhi mikononi mwa Mwenyezi Mungu ambaye anamlinda na kumsimamia. Anasema katika utume wake kuna kazi kubwa na nyingi ambazo ziko mbele yake kama kwa wanafunzi wanaoteseka wakati wanapokaribia kufanya mitihani yao ya kufunga mwaka wa masomo. Anasikitika sana moyoni mwake pale vyombo vya habari vinavyopotosha ukweli wa mambo kwa faida zao. Kuhusiana na Argentina anasema kwa sasa hafuatilii sana mageuzi yanayotendeka huko. Ni nchi ambayo ina nafasi na fursa nyingi lakini bado hazijatumiwa kikamilifu.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, maskini ni amana na kiini cha Injili, bila ufukara, Injili inakosa radha ya maisha. Saratani kubwa zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ni: umaskini, rushwa, ufisadi na biashara haramu ya binadamu. Ili kufanikisha mapambano dhidi ya majanga yanayomwandama mwanadamu kuna haja ya kuzingatia mambo makuu matatu: kumbu kumbu, uwezo wa kuangalia yaliyopo na ndoto kwa siku za usoni. Baba Mtakatifu Francisko anasema angependa kukumbukwa na wengi kama mtu anayejitahidi kutenda mema na wala hakuna cha zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.