2015-05-26 09:57:00

Kongamano la uchumi wa mshikamano linafanyika, CUEA, Nairobi, Kenya


Takwimu za Benki ya Dunia zinaonesha kwamba, uchumi wa nchi zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara unakua kwa asilimia 6% na kwamba, hili ni eneo ambalo limeendelea kuwa ni kivutio kikuu cha wawekezaji wa ndani na nje ya Bara la Afrika. Lakini umaskini wa hali na kipato, pengo kubwa kati ya maskini na matajiri pamoja na ukosefu wa usawa katika masuala ya kijamii ni mambo ambayo kamwe hayawezi kukubalika.

Kiwango cha kima cha chini cha mshahara hakiwezi kukidhi gharama ya maisha ya wananchi wengi Barani Afrika. Bei ya mazao ya wakulima ni ndogo sana ikilinganishwa na bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya Bara la Afrika. Unyonyaji ni kati ya  mambo ambayo yanaendelea kuwatendea watu wengi. Ni maneno ya Professa Betty Njagi, Jaalim kutoka katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashariki na Kati, CUEA anapojaribu kuweka mazingira ya ukuaji wa uchumi Barani Afrika, kama sehemu ya maandalizi ya Kongamano la kimataifa kuhusu uchumi wa mshikamano, linalofanyika Jijini Nairobi kuanzia tarehe 27 hadi tarehe 31 Mei 2015.

Kwa upande wake Professa Luigino Bruni, mwanachama wa Tume ya Kimataifa ya Uchumi na mshikamano ambaye pia ni Jaalim wa Uchumi katika Chuo kikuu cha LUMSA, kilichoko mjini Roma anasema, kongamano hili linalenga pamoja na mambo mengine kupembua umoja na ugunduzi; mambo msingi yanayowezesha uchumi kuendelea kukua, changamoto kwa ukuaji wa uchumi Barani Afrika. Kongamano hili ni matokeo ya kongamano lililofanyika kunako mwaka 2011 nchini Brazil na Kenya.

Kongamano la mwaka huu linataka kutoa nafasi ya pekee kwa Waafrika kushiriki kikamilifu kama anavyobainisha Geneviève Sanze. Zaidi ya wajumbe 421 kutoka katika nchi 41 wanashiriki katika kongamano hili, ambalo limetanguliwa na semina ya kimataifa iliyowajumuisha wafanyabiashara vijana kutoka katika nchi za Kiafrika. Vijana hawa wanaonesha umuhimu wa wafanyabiashara Barani Afrika kushirikiana kwa dhati. Uchumi wa mshikamano ni dhana iliyoanzishwa na Mama Chiara Lubich kunako mwaka 1991 huko Brazil, ili kusimama kidete katika mapambano dhidi ya umaskini, kwa kuwajengea watu uwezo wa kiuchumi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.