2015-05-26 15:05:00

Inasikitisha sana kumwona Mkristo amemezwa na kutawaliwa na malimwengu!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri aliyotoa kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne tarehe 26 Mei 2015 amewataka waamini kuhakikisha kwamba, wanamfuasa Kristo kwa moyo wao wote na kamwe wasikubali kumezwa na malimwengu, kwani haiwezekani kwa Mkristo kuishi nusu nusu. Mtakatifu Petro katika mahojiano maalum na Yesu, anamuuliza, Je, wao watapata nini kwa kuacha yote, swali ambalo liliulizwa baada ya Yesu kutoa majibu yaliyomkatisha tamaa yule kijana tajiri, akaondoka kwa huzuni kwa sababu alikuwa anamiliki mali nyingi, lakini mchoyo kiasi cha kushindwa kuwagawia maskini.

Baba Mtakatifu anasema, jibu la Yesu linatoa mwelekeo tofauti kabisa na mambo ambayo Mitume walitegemea kusikia. Anawaambia kwamba, wataweza kuurithi Ufalme wa Mungu, lakini pia watakumbana na dhuluma pamoja na Misalaba katika hija ya maisha yao. Mkristo hana budi kufanya maamuzi machungu katika hija ya maisha yake kwa kuamua kumfuasa Kristo kwa moyo na akili zake zote; kwa kujikana na hatimaye, kujitwika vyema Msalaba na kisha kumfuasa Yesu.

Ujio wa Roho Mtakatifu kwa Mitume wa Yesu, uliwatakasa na mawazo kuhusu ukuu, kiasi cha kukumbatia moyo wa sadaka na majitoleo kwa ajili ya upendo kwa Yesu Kristo, kwani hapa hakuna njia ya mtakato yaani: mali na malimwengu; ufukara na ufuasi wa Yesu. Uchu wa mali, anasa na kiburi ni mambo ambayo yanawafanya wakristo kuwa mbali na Yesu, lakini wanapaswa kutambua kwamba, wakwanza watakuwa wa mwisho na wale wa mwisho watakuwa wa kwanza, changamoto ya kuwa kweli ni wahudumu wa maskini.

Wakristo waoneshe moyo wa kuhudumia kama alivyofanya Kristo mwenyewe katika maisha yake; ikiwa kama mtu amebahatika kupata mali na utajiri, basi autumie kwa ajili ya huduma, kwani Yeye alikuja ulimwenguni ili kuhudumia na wala si kuhudumiwa na kutoa maisha yake ili yawe ni fidia wengi. Yesu anawataka wafuasi wake kujenga na kuimarisha fadhila ya unyenyekevu katika maisha yao. Haipendezi kabisa kumwona Mkristo amemezwa na malimwengu. Wale ambao wameacha yote kwa ajili ya Yesu, atawakirimia Msalaba na maisha ya uzima wa milele.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.