2015-05-25 12:03:00

Wananchi wa Burundi: Dumisheni haki, amani, utulivu na majadiliano!


Hali ya kisiasa na kiusalama nchini Burundi inaendelea kuwa tete kila kukicha na kwamba, bado kuna umati mkubwa wa wanachi wanaoendelea kuandamana mitaani kumpinga Rais Peirre Nkurunziza kuwania tena madaraka kwa awamu ya tatu, jambo ambalo wengi wanasema ni ukiukwaji wa Katiba, ambayo kimsingi ni Sheria mama. Bwana Ban Ki-Moon, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa pamoja na viongozi mbali mbali wanaendelea kuitaka Serikali ya Burundi pamoja na wapinzaji kuendeleza mchakato wa majadiliano pamoja na kusitisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Jumuiya ya Kimataifa inalaani mauaji ya Bwana Zedi Feruzi, kiongozi wa Chama cha Upinzani cha UDP, aliyeuwawa mwishoni mwa juma mjini Bujumbura. Juhudi za Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kutaka pande zote mbili kuendeleza majadiliano, ili kukomesha machafuko ya kisiasa nchini Burundi bado hazijazaa matunda yanayokusudiwa. Umoja wa Mataifa unawataka wananchi wa Burundi kujenga na kuimarisha mchakato wa amani.

Itakumbukwa kwamba, uchaguzi mkuu wa Rais unatarajiwa kufanyika hapo tarehe 26 Juni wakati ambapo uchaguzi wa Wabunge na Madiwani unatarajiwa kufanyika tarehe 5 Juni 2015. Kwa sasa kuna wimbi kubwa na wananchi wa Burundi wanaokimbia ili kusalimisha maisha na mali zao.

Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi linasema kwamba, ikiwa kama hali ya usalama inaendelea kuwa tete kiasi hiki, Kanisa halitaunga mkono agenda ya kuendelea na mchakato wa uchaguzi kwani hautakuwa huru wala wa haki na kwamba, itakuwa vigumu kwa wananchi wa Burundi kuweza kukubali matokeo na hapo unaweza kuwa ni mwanzo wa machafuko makubwa ya kisiasa.

Maaskofu wanaitaka Serikali kuhakikisha kwamba, uhuru wa vyombo vya habari unaheshimiwa na wananchi kutulia na kutafuta muafaka wa tatizo hili kwa njia ya majadiliano, haki na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.