2015-05-25 13:11:00

Umoja wa Wakatoliki unaimarishwa kwa kushikamana na Khalifa wa Mt. Petro


Kila mwaka ifikapo tarehe 24 Mei, Kanisa linaadhimisha kumbu kumbu ya Bikira Maria msaada wa Wakristo. Kunako mwaka 2007, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alianzisha Siku maalum kwa Kanisa kwa ajili ya kuombea Wakristo nchini China. Kardinali Pietro Parolin Katibu mkuu wa Vatican anasema kwamba, umoja miongoni mwa waamini wa Kanisa Katoliki unaimarishwa na kudumishwa kwa kuungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii ni haki ya kila mwamini na kamwe haipaswi kubezwa.

Hivi karibuni, Rais wa China XI Jinping akizungumza na waandishi wa habari alisikika akisema kwamba, watu kutoka nje ya China hawana ruhusa ya kuingilia masuala ya kidini nchini China. Kardinali Parolin akihojiwa na Shirika la Habari la ANSA anatumaini kwamba, maneno haya hayatakuwa ni kikwazo katika mchakato wa majadiliano kati ya China na Vatican.

Kardinali Parolin akihojiwa na Kituo cha Televisheni cha Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, TV2000 anasema kwamba, uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na China pamoja na Vietnam ni jambo ambalo halina haraka sana, linaendelea kushughulikiwa kwa uvumilivu na kwamba, yote haya yataweza kuzaa matunda kwa wakati wake.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI wakati anatangaza siku hii alikazia kwa namna ya pekee umoja na mshikamano kati ya Wakatoliki nchini China pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Wakatoliki sehemu mbali mbali za dunia wanahimizwa kwa namna ya pekee kusali kwa ajili ya kuombea umoja, udugu, mshikamano na ushirikishwaji wa wote, ili Wakatoliki nchini China waweze kujisikia kuwa karibu na ndugu zao katika Kristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.