2015-05-25 15:01:00

Papa aonya; uchoyo huzaa rushwa na magendo


Ni muhimu kila mtu kushirikiana na wengine katika masuala ya utajiri, ili utajiri huo uwe kwa ajili ya manufaa ya wengi. Maisha ya kupenda kujikusanyia mali kibinafsi, hayo ni maisha yaliyojaa ubinafsi na roho mbaya. Ni kuishi bila kuwa na  tumaini thabiti kwa siku za baadaye. Moyop wa aina hiyo, Papa anasema hujenga aina zote za rushwa, iwe katika mambo makubwa au madogomadogo. Papa Francisko ametoa onyo hilo,  wakati wa homilia yake, mapema asubuhi Jumatatu hii, katika Kanisa dogo la Mtakatifu Marta, ndani ya Vatican .  

Tafakari ya Papa ililenga kufafanua maana ya mfano wa ngamia na tundu la sindano, akionyesha jinsi shauku  ya mtu inavyoweza badilika kwa haraka,   kutokana na hofu zinazotokana na ubinafsi wa kutotaka kushirikiana na wengine yale aliyojaliwa.  Homilia ya Papa inalenga katika tukio la Yesu alipokutana na kijana tajiri,  anayeuliza afanye nini ili aweze kuandamana naye, baada ya kueleza kwamba anaziishi amri zote za Mungu. Kijana huyo mara hisia na mtazamo wake ulibadilika katika hatua ya mwisho alipoambiwa na Yesu “nenda kauze vyote ulivyo navyo na wape maskini,  kisha njoo kunifuata”. Ghafla, "furaha na matumaini" ya kijana tajiri vilitoweka  kabisa, kwa sababu kwake yeye ilikuwa vigumu kutengana na mali zake.

Papa anautazama moyo wa kijana huyo tajiri na kusema, unaotoa somo kwetu sote kwamba, kushikamana sana na utajiri, unakuwa ni mwanzo wa kujenga vishawishi katika kila njia,  ili kuweza kujipatia kila linalowezekana hata kwa njia zisizo halali, njia ya utoaji wa rushwa na magendo,bila kujali athari zake kwa maisha ya wengine. Papa alieleza kwa kutazama hali halisi za rushwa, ubinafsi, na hongo vilivyotandaa  kila mahali, mpaka ndani ya biashara, mtu akijaribu kumpunja mwingine kwa makusudi,  rushwa  katika siasa, elimu, ajira, tiba , kanisa  na huduma zote za kijamii, akihoji kwa nini iwe? Ni kutokana na maisha ya kutaka sifa zinazoshikamana na uwezo  binafsi kihali na mamlaka,  ingawa watu hao ni waamini. Papa anasema kama ilivyokuwa kwa kijana huyo aliyesema anazishika amri zote za Mungu, lakini alikuwa bado amefungwa na ubinafsi, na upeo wake wa  macho haukuona mbali, na hivyo hakuwa anaishi kwa matumaini  kwa siku za baadaye. Maisha yake yaliyojengwa katika mali,  na kumfanya asahau kwamba, yote ya kidunia tunayaacha hapa duniani.

Papa aliendelea, kuzungumzia siri katika milki ya mali, akisema , Utajiri na uwezo wa kushawishi na kujenga upotofu wenye kutufanya kuamini kwamba, utajiri hufanya yote kuwa mazuri , kuwa na maisha ya peponi, lakini kumbe hiyo ni mbingu bandia, inayotoweka mara. Ni sawa na mtu tajiri aliyeficha mali yake akifikiri atakuwa nayo daima na kumbe wezi wakaja na kuichukua yote na kumwacha mikono mitupu.

Papa ameyataja maisha ya kutegemea utajiri wa dunia hii, kuwa ni maisha yenye mashaka na hofu, yasikuwa na tumaini la kweli kwa siku za baadaye . NI maisha batili. Na aliweka bayana, anapozungumzia mtu kushikamana na utajiri haina maana ya kutokuwa na mipango mizuri ya kusimamia mali vizuri.Lakini ni kinyume chake , kutoshikamana na utajiri ina maana ya kuwa na mipango  mizuri ili mali hiyo iweze kutumika kwa manufaa ya wote. Na kwamba,Bwana hujalia baadhi ya watu nafasi ya kuwa tajiri, kwa kuwa anapenda majaliwa hayo,  iwe kwa manufaa ya wote, wala si kwa ajili mtu mwenyewe binafsi . Lakini mara kwa mara inakuwa tofauti, wengi waliojaliwa, huufunga moyo wao kibinafsi, wakijenga hali ya kutaka kujilimbikiza zaidi na zaidi hata kwa njia za kugandamiza wengine kwa njia ya rushwa na hongo. Huufunga mkono  na  upeo wa macho.

Papa aliendelea kusisitiza , utajiri bila ukarimu, humwongoza mtu kusadiki ana uwezo kama Mungu. Na hatima yake ni hunyausha wema wake  na matumaini yake. Yesu alimalizia na maneno,  'Heri walio maskini wa  roho', akiwa na maana ya heri walioufuta moyo wa kushikamana na utajiri wa dunia hii , maana kwa kufanya hivyo, Bwana atawapa utajiri mwingi zaidi,  kwa manufaa ya wote.  

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.