2015-05-24 10:57:00

Utengano ni donda kubwa katika Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa


Katika maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste Jimbo Katoliki la Phoenix, Marekani kwa kushirikiana na “Chama cha John 17” kilichoanzishwa na Joe Tosini, Mchungaji wa Kanisa la Kipentekoste kilichoko nchini Marekani, wameadhimisha siku ya Umoja wa Wakristo, uliokuwa unaongozwa na kauli mbiu  ya sala ya Yesu “Baba wote wawe na umoja”. Tukio hili la Kipentekoste limehudhuriwa na Wakristo kutoka katika Makanisa na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya tukio hili amewapelekea ujumbe wa Video ili kuwashukuru na kuwapongeza kwa kujikita katika mchakato wa upatanisho ili wote wawe wamoja chini ya Kristo, kwa kukutana na kusali pamoja, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia neema ya umoja. Anaungana nao katika hija ya maisha ya kiroho, ili kusali kwa ajili ya kuombea umoja wa Wakristo unaopata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo. Hii ni hija ya sala, kazi ya pamoja na kusaidiana kama ndugu katika Kristo.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, utengano kati ya Wakristo ni donda kubwa katika Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Wakristo wanataka kuponya donda hili kwani ni kazi ya Shetani, Baba wa ubaya na kinzani anayetaka kuona Wakristo wakiendelea kugawanyika. Anawataka wote kwa pamoja kuungana ili kumwomba Roho Mtakatifu aweze kuwajalia neema ya umoja ili dunia ipate kuamini kwa njia ya ushuhuda unaotolewa kwa damu ya Wakristo inayoendelea kumwagika sehemu mbali mbali za dunia pasi na ubaguzi. Huu ndio Uekumene wa Damu.

Baba Mtakatifu anakiri kamba umoja wa Wakristo kamwe hautajengwa na wanataalimungu kwani wao ni wasaidizi tu, kazi kubwa inafanywa na Roho Mtakatifu pamoja na Wakristo wenyewe kuweka nia ya dhati na kutambua kwamba, Yesu ni Bwana. Roho Mtakatifu awajalie kujenga na kuimarisha amani n aumoja kati ya wafuasi wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.