2015-05-24 07:54:00

Mwenyeheri Oscar Romero chachu ya ujenzi wa amani, msamaha na upatanisho


Mwenyeheri Askofu mkuu Oscar Arnulfo Romero Galdamez alikuwa ni mchungaji mwema aliyejitahidi kujenga na kudumisha amani kwa nguvu ya upendo, akashuhudia imani kwa Kristo na Kanisa lake kiasi hata cha kuyamimina maisha yake. Mwenyezi Mungu anaendelea kuwakumbuka watu wake na kuwakomboa kutoka katika dhuluma na nyanyaso, ili waweze kutangaza na kulitukuza jina lake. Mwenyezi Mungu ataendelea kuwapatia watu wake wachungaji wapendezao moyo wake, watakaowalisha kwa maarifa na fahamu.

Hizi ni sababu msingi ambazo Baba Mtakatifu Francisko anamwelezea Askofu mkuu Josè Luis Escobar Alas wa Jimbo kuu la San Salvador, ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu katoliki El Salvador  kwa nini ameamua kumtangaza Askofu mkuu Oscar Romero kuwa Mwenyeheri. Alikuwa ni kiongozi mchapa kazi, aliyeonesha upendo mkuu kwa Mungu, akawaongoza watu wake kama Kristo mchungaji mwema. Alijitahidi kuwaongoza, kuwalinda na kuwatunza watu wake aliokuwa amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu. Akawa mwaminifu kwa Injili kwa kuonesha umoja na mshikamano kwa Kanisa zima.

Mwenyeheri Oscar Romero alitoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Wakati alipokuwa anaadhimisha Fumbo la upendo na upatanisho, akapata neema ya kujitambulisha kama Yesu mwenyewe aliyejisadaka kwa ajili ya binadamu. Kutangazwa kwake kuwa ni Mwenyeheri ni kielelezo cha furaha kubwa kwa taifa na mataifa ya Amerika ya Kusini, kwani Mwenyezi Mungu amemwezesha Askofu mkuu Oscar Romero kuona na kusikiliza kilio cha watu wake na kushuhudia upendo wa Kikristo.

Sauti ya Mwenyeheri Oscar Romero ni mwaliko kwa Familia ya Mungu kujenga na kuimarisha mshikamano wa dhati, kwani imani kwa Kristo ni kikolezo cha ujenzi wa Jumuiya inayosimikwa katika amani na mshikamano, changamoto ya Wakristo wote kujichotea utajiri wa huruma ya Mungu, chachu ya upatanisho ndani ya jamii. Ni mwaliko wa kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai kwa kukataa kishawishi cha kukataa uhalifu na chuki, ili kujikita katika upendo ambao Yesu mwenyewe aliouonesha pale juu Msalabani.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, huu ni mwaliko wa kushinda kishawishi cha ubinafsi, ukosefu wa usawa na ukatili kati ya watu, ili kuonja umaskini na kwamba, viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa wanao wajibu wa kugeuza silaha kuwa ni vyombo vya kazi. Baba Mtakatifu anawatakia heri na baraka wale wote wanaomkimbilia Mwenyeheri Oscar Romero katika shida na mahangaiko mbali mbali na kwamba, huu ni wakati wa upatanisho wa kitaifa ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kwa wakati huu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.