2015-05-23 15:09:00

Saidieni kujenga usawa na mshikamano kati ya watu kwa kutengeneza ajira


Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi, tarehe 23 Mei 2015 Katika kumbu kumbu ya maadhimisho ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Shirikisho la Wafanyakazi Wakristo Italia, ACLI, amekutana na wanachama wa Shirikisho hili kwa kukazia mambo makuu manne yanayohusiana na masuala ya kazi: Uhuru, Ugunduzi, Ushirikishwaji na mshikamano; mambo ambayo yamekuwa ni kiini cha dhamana na utume wao; tayari kuangalia changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo hususan kwa uwepo mkubwa wa mipasuko ya kijamii, ili kujenga usawa na mshikamano kati ya watu.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, leo hii kuna umati mkubwa wa watu wasiokuwa na fursa za ajira; wengine wanaendelea kufanyishwa kazi za suluba kwa ujira mdogo; mambo yanayowaathiri kwa namna ya pekee, vijana wa kizazi kipya. Ukosefu wa fursa za ajira unadhalilisha utu wa binadamu, unakwamisha utimilifu wake, mambo ambayo yanapaswa kushughulikiwa kikamilifu.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, uhuru wa kweli unapata chimbuko lake katika kazi ambayo muasisi wake ni Mungu mwenyewe. Mwanadamu anashiriki na kuendelea kumwilisha kazi ya uumbaji inayomwilishwa katika historia ya mwanadamu. Lakini kwa bahati mbaya, kazi imekuwa ni chanzo cha nyanyaso na dhuluma katika ngazi mbali mbali za maisha ya mwanadamu; kazi zinatekelezwa katika mfumo wa utumwa kwa kuwanyanyasa maskini zaidi; athari za uchumi zinawafanya watu wengi kutokuwa na kazi bora na hivyo kushindwa kuonja uzuri na amani katika kazi. Kazi inapaswa kuwa ni kielelezo cha matumaini na maisha mapya.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, kila mwanadamu anacho kipaji cha ugunduzi ambacho Mwenyezi Mungu amemkirimia. Ikiwa kama kipaji hiki kitatumika kwa ajili ya mafao ya wengi na kwa kushirikiana na jirani zake, kitasaidia kukuza uchumi na kujenga maisha ya kijamii. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, vijana wanapewa fursa ya kushirikisha karama na mapaji yao sanjari na kuondokana na mambo ambayo yanawakwamisha kutoingia mapema iwezekanavyo katika ulimwengu wa wafanyakazi.

Baba Mtakatifu anawataka wafanyakazi kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa kushirikiana na kuwajibika pamoja na wengine, kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi ili kuondokana na tabia ya ubinafsi, kama kielelezo cha mwendelezo wa kazi ya Mungu kwa ajili ya binadamu wote. Hapa kuna haja ya kujenga na kuimarisha mshikamano na watu ambao wanakosa fursa za ajira.

Hii ni dhamana inayoweza kutekelezwa kwa umakini mkubwa na Shirikisho la Wafanyakazi Wakristo Italia kwa kujenga utamaduni wa watu kukutana na kuonjeshana ukarimu pamoja na kuwapatia ujuzi na maarifa ili waweze kuchangia katika mchakato wa uchumi. Uhuru, ugunduzi, ushirikishaji na mshikamano ni sehemu ya vinasaba vya Shirikisho hili; tunu zinazopaswa kumwilishwa kwa ajili ya mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu amewaambia wajumbe wa Shirikisho hili kwamba, wanapaswa kuanza kujiwekea mikakati ya kuwahudumia wanachama wao ndani na nje ya Italia kufuatia wimbi kubwa la wananchi wa Italia wanaotafuta fursa za ajira nje ya Italia. Wao wawe ni kielelezo cha wananchi wengi wa Italia ambao kwa miaka mingi walihama na kwenda kutafuta maisha bora sehemu mbali mbali za dunia. Wasimame kidete kupambana na baa la umaskini wa hali na kipato linaloendelea kuwanyemelea wananchi wengi wa Italia.

Kutokana na uzee, magonjwa, ongezeko la mtoto katika familia pamoja na kukosekana kwa fursa za ajira, watu wanajikuta wakitumbukia kwenye umaskini. Ikumbukwe kwamba, uwekezaji katika masuala ya kijamii kwani hii ni miundo mbinu inayoweza kukoleza ukuaji wa uchumi kwa gharama nafuu. Wajitahidi kuwa waratibu wa mapambano dhidi ya umaskini, kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha utu na ubora wa kazi. Shirikisho hili liendelee kuwa aminifu kwa wafanyakazi, demokrasia na Kanisa, lakini zaidi waaminifu kwa maskini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.