2015-05-22 15:34:00

Yesu akamwangalia Petro: Akamchagua: Akatokwa chozi zito: Akapewa utume!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Ijumaa, tarehe 22 Mei 2015 amejikita katika mahojiano kati ya Yesu na Mtakatifu Petro; mahojiano ambayo yalimkumbusha Mtakatifu Petro historia ya hija ya maisha yake, Yesu alipomwangalia, akampenda, akamchagua na kukabidhi dhamana ya kuchunga Kondoo wake.

Yesu kwa mara ya kwanza alipokutana na Andrea alikwenda moja kwa moja kwa ndugu yake Petro, akamwambia kwamba, wamemwona Masiha na walipokutana na Yesu, akamwangalia kwa jicho la upendo na hatimaye akamwambia, Wewe Simoni mwana wa Yohane, tangu sasa utaitwa Kefa, maana yake Petro, au Mwamba. Macho ya Yesu yanajikita katika utume na hapa Petro anafurahi kwa dhamana anayokabidhiwa, kiasi cha kuacha yote na kuanza kumfuasa Yesu.

Baba Mtakatifu anaendelea kutafakari juu ya hatua ya pili, Yesu alipomwangalia Mtakatifu Petro, Siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, katika kimya kiuu, pale Petro alipomkana Yesu mara tatu na mara jogoo akawika, Yesu akamwangalia, Petro, akatoa machozi ya toba na wongofu wa ndani; mambo yaliyomwimarisha katika hija ya maisha yake kama mfuasi wa Kristo, akitambua utajiri na mapungufu yake kama binadamu.

Mara ya tatu, Yesu alimwangalia Mtakatifu Petro baada ya ufufuko wake, akamwimarisha katika utume na kumtaka aendelee kuwachunga Kondoo wake, lakini kabla ya yote alitaka kuwa na uhakika wa upendo wa Petro ambao ulipaswa kububujika kutoka katika undani wa moyo wake, ndiyo maana Yesu alimuuliza mara tatu! Petro, akashikwa na kwikwi! Lakini, huu ulikuwa ni mwanzo tu wa Njia ya Msalaba, ambayo ingehitimishwa kwa ushuhuda wa kuyamimina maisha yake kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini kwamba, Yesu daima anaangalia kwa jicho la upendo, ana uwezo wa kusamehe na kuendelea kukabidhi utume ambao unapaswa kutekelezwa kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Hii ni changamoto kwa waamini kutafakari katika undani wao, kwa kujuta, kutubu na kumwongokea Mungu kutokana na dhambi zao, tayari kuomba moyo wa ujasiri, ili kusonga mbele katika utekelezaji wa utume ambao wamekabidhiwa na Mama Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.