2015-05-21 15:47:00

Wanawake wameamua kujifunga kibwebwe katika mchakato wa maendeleo endelevu


Mwaka 2015 ni muhimu sana kwa Umoja wa Mataifa, kwani Jumuiya ya Kimataifa inaanza mchakato wa majadiliano ya kuangalia vipaumbele baada ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia kwa mwaka 2015. Lengo ni kuibua mbinu mkakati wa maendeleo endelevu, mambo msingi ambayo yanaathari kubwa kwa ustawi na maendeleo ya wanawake duniani.

Kunako mwaka 2009 kulifanyika mkutano wa kimataifa kuhusu: maisha, familia na maendeleo; mkutano ulioandaliwa kwa ushirikiano kati ya Baraza la Kipapa la haki na amani, Shirikisho la Kimataifa la Wanawake kwa ajili ya maisha na familia, WWALF pamoja na Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO.

Mwaka huu, kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 24 Mei, wanawake hawa wanafanya mkutano wao hapa mjini Roma kwa kuwahusisha wanawake mbali mbali ambao wako mstari wa mbele katika kutetea utu na heshima ya wanawake duniani. Kati ya mada zinazofanyiwa kazi ni: Wanawake rasilimali muhimu katika mabadiliko; Utumwa mamboleo; wanawake na kazi; Ekolojia ya binadamu, utu na heshima ya binadamu; elimu na kazi; umaskini na maendeleo.

Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani akizungumza na waandishi wa habari mjini Vatican siku ya Alhamisi, tarehe 21 Mei 2015 amekazia dhamana na nafasi ya wanawake katika medani mbali mbali za maisha sanjari na kujenga ushirikiano na mfungamano na wanaume ili kukamilishana. Wanawake wawe mstari wa mbele katika majadiliano ya kidini na kiekumene, daima wakijitahidi kuwa ni vyombo na wajenzi wa amani.

Ulimwengu mamboleo umesheheni pia utumwa mamboleo, nyanyaso na dhuluma dhidi ya wanawake, mambo ambayo yanatishia utu na heshima ya wanawake. Bado kuna wimbi kubwa la biashara haramu ya binadamu na waathirika wakubwa ni wasichana na wanawake; mambo ambayo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu. Kuna ndoa za shuruti na sasa kumeibuka tatizo la kisayansi la kuwabebesha wanawake mimba kwa ajili ya watu wengine. Yote haya ni mambo ya kuangalia, ili kuweka mikakati ya maendeleo endelevu kwa miaka ijayo.

Mheshimiwa Olimpia Tarzia Mwenyekiti wa Shirikisho la Kimataifa la Wanawake kwa ajili ya maisha na familia, WWALF katika hotuba yake anakazia umuhimu wa wanawake kusimama kidete kutetea haki msingi za binadamu; utu na heshima ya binadamu kwa kupambana na baa la umaskini na njaa duniani; kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kutangaza Injili ya Uhai; kanuni maadili na utu wema.

Kwa upande wake, Professa Maria Giovanna Ruggieri Mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, amegusia kuhusu umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kudumisha Injili ya Familia; kuwasikiliza, kuwasaidia na kuthamini mchango wa vijana katika mchakato wa maendeleo pamoja na kupambana na umaskini wa haki na kipato.

Na Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.