2015-05-21 15:36:00

Umoja na mshikamano ni changamoto endelevu miongoni mwa Wakristo!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 21 Mei 2015, amekazia kwa namna ya pekee Sala ya Yesu anayemwomba Baba yake wa mbinguni kudumisha umoja miongoni mwa wafuasi wake kama wao walivyo wamoja. Hii ni changamoto kwa Wakristo kupambana ili kuvunjilia mbali kinzani na migawanyiko; vita na wivu usiokuwa na mashiko. Yesu alisali sala hii siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, akakazia umoja na mshikamano kama kielelezo cha ushuhuda wa wafuasi wake.

Baba Mtakatifu anaendelea kukumbusha kwamba, Yesu alisali na kuwaombea wote ambao watamwini kwa sababu ya Neno la mitume wake, ili wote wawe na umoja kama wao walivyo wamoja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Haya ni maneno ambayo Wakristo kwa miaka mingi wamekuwa wakiliyasikiliza, lakini bado hawajayapatia uzito wa kutosha. Wakristo wanakumbushwa kwamba, utengano ni kati ya madonda makuu ambayo Yesu mwenyewe ameyagharimia kwa Damu yake azizi.

Yesu anasali kwa ajili ya umoja na mshikamano wa Watu wake, Umoja wa Kanisa dhidi ya kinzani, magovi, vita na wivu ambao unajionesha kwa namna ya pekee hata katika maisha ya kifamilia, miongoni mwa watawa, majimboni na hata katika Kanisa la Kiulimwengu. Hiki ni kishawishi kikubwa na kinapaswa kushindwa kwa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa umoja, ili wote waweze kuwa wamoja, changamoto endelevu kwa Wakristo wote.

Kamwe Wakristo wasikubali kutumbukizwa kwenye utengano, bali wajitahidi kutafuta, kujenga na kudumisha umoja, msamaha na upatanisho. Kanisa linahitaji kumwilisha sala ya kuombea umoja wa Wakristo katika maisha na utume wake. Umoja wa Wakristo unapata chimbuko lake katika neema, kwa kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu, ili kutenda na hivyo kuwasaidia wakristo kubaki wakiwa wameungana na Yesu, tayari kushiriki naye katika maisha ya uzima wa milele, ili kutafakari pamoja naye, ule utukufu wa Baba yake wa mbinguni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.