2015-05-21 15:21:00

Mwenyeheri Askofu mkuu Oscar Romero: Kioo cha maisha na utume wa Kipadre


Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, tarehe 23 Mei 2015, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Askofu mkuu Oscar Romero kuwa Mwenyeheri. Itakumbukwa kwamba, aliuwawa kikatili tarehe 24 Machi 1980 wakati alipokuwa anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Mwenyeheri mtarajiwa ni kiongozi anayefahamika sana ndani na nje ya San Salvador.

Baba Mtakatifu Francisko anamtambulisha Askofu mkuu Oscar  Romero kuwa kiongozi anayetoa muhtasari wa maisha na utume wa Kipadre. Ni Askofu na mfiadini; mchungaji mwaminifu kadiri ya Moyo Mtakatifu wa Yesu; Mwinjilishaji na Baba wa maskini; Shuhuda amini wa ujenzi wa ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, amani, udugu na mshikamano. Alikuwa ni Padre mwema na Askofu mwenye hekima na busara, aliyejaliwa na Mwenyezi Mungu fadhila mbali mbali katika maisha yake.

Askofu mkuu Oscar Romero alimpenda Yesu, akakuza na kudumisha ndani mwake Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu; akalipenda na kulipigania Kanisa la Kristo; akaonesha Ibada ya pekee kabisa kwa Bikira Maria. Mwenyeheri mtarajiwa Askofu mkuu Oscar Romero aliwapenda upeo watu wake. Ushuhuda wake wa kifodini ulikuwa ni mchakato wa muda mrefu, tangu akiwa Mseminari mdogo, alijiandaa kujikabidhi mikononi mwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sadaka ya maisha yake, akawa daima anamwomba Mwenyezi Mungu kumsaidia na kumsindikiza katika safari hii ndefu ya maisha yake.

Huu ni ushuhuda unaotolewa na Kardinali Angelo Amato, katika mahojiano maalum na Radio Vatican. Anasema ni kiongozi ambaye aliwavuta wengi kutokana na toba na wongofu wa ndani katika maisha yake. Kwa namna ya pekee anakumbukwa jinsi ambavyo alimlilia na kumwombolezea Padre Rutilio Grande, aliyeuwawa kikatili tarehe 12 Machi 1977, aliyekuwa ameacha kufundisha kama Jaalim wa Chuo kikuu, ili kujisadaka maisha yake kwa ajili huduma kwa maskini na wale waliokuwa wanaonewa.

Askofu mkuu Oscar Romero katika mahubiri yake kwa mazishi ya Padre Rutlio Grande alimkumbuka kwa kusema kwamba, alikuwa ni kiongozi wa Kanisa aliyehubiri kuhusu imani, uhuru na maisha ya uzima wa milele. Huu ni uhuru unaofumbatwa katika furaha ya maisha ya uzima wa milele; uhuru unaobubujika kutoka katika moyo wa toba na majuto dhidi ya dhambi, ni uhuru unaojikita katika Kristo, nguvu ya pekee inayomwokoa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Askofu mkuu Oscar Romero alisimama kidete kuwalinda na kuwatetea wanyonge pamoja na Kanisa, kiasi cha baadhi ya watu kujenga chuki na uhasama dhidi yake. Lakini yeye aliendelea kuonesha moyo upendo, huruma, msamaha na amani; akawa tayari kukumbatia maisha ya mbinguni. Alitoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, ndiyo maana anakumbukwa na wengi kama “Baba wa maskini na mtetezi wa wanyonge”. Alihubiri toba na wongofu wa ndani; huruma na msamaha pamoja na kutenda haki.

Kardinali Angelo Amato anabainisha kwamba, Mwenyeheri mtarajiwa Oscar Romero ni kielelezo cha utakatifu wa maisha kutoka Amerika ya Kusini. Huko Kanisa anasema Baba Mtakatifu Francisko limebahatika kupata mifano ya watakatifu ambao wamejitahidi kumwilisha imani na upendo wao kwa Kristo na Kanisa lake katika uhalisia wa maisha na utume wao, wakawa tayari kujisadaka kwa ajili ya kuwatangazia Watu wa Mataifa upendo na huruma ya Mungu.

Watakatifu hawa ni kama Fra Junipero Serra atakayetangazwa kuwa Mtakatifu tarehe 23 Septemba 2015, huko Washington, DC, Marekani wakati wa hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Marekani. Wengine ni: Rosa wa Lima, Mariana wa Quito, Teresia de los Andes; Toribido wa Magroyevo; Francois de Laval; Martin de Porres, Alberto Hurtado; Francesca Cabrini, Elizabeth Ann Seaton na Catalina Drexel. Wengine ni: Francisco Solano, Josè de Anchieta, Alonso de Berzana, Maria Antonia de Paz y Figueroa; Jose Gabriel wa Rozari Brochero pamoja na mashuhuda wa imani kama vile Roques Gonzales, Miguel Pro na Oscar Armulfo Romero.

Lakini kuna umati mkubwa wa watakatifu na wafiadini wanaoendelea kusali kwa ajili ya ndugu zao ambao bado wanasafiri hapa dunia. Mwenyeheri Oscar Romero ni kati ya kundi hili kubwa linalomwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao yanayoonesha uaminifu katika mchakato wa Utangazaji wa Injili ya Kristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.