2015-05-21 16:41:00

Balozi Joel Musa Nhleko awasilisha hati za utambulisho mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 21 Mei 2015 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Bwana Joel Musa Nhleko, Balozi wa Swaziland mjini Vatican. Balozi Nhleko alizaliwa kunako tarehe 2 Februari 1948 ameoa na ana watoto wawili. Alipata masomo yake ya juu katika masuala ya fedha kutoka katika Chuo Kikuu cha St. John, New York, Marekani kunako mwaka 1992. Akajiendeleza zaidi na kupata Shahada ya uzamivu katika uwanja wa siasa na masuala ya uongozi kutoka Chuo Kikuu cha St. John New York, Marekani kunako mwaka 1993.

Katika maisha yake amewahi kuwa mfanyakazi katika Benki ya Standard Charter kati ya mwaka 1974 hadi mwaka 1984. Akaajiriwa hazina kunako mwaka 1984 hadi mwaka 1987. Kunako mwaka 1987 hadi mwaka 1992 akahamishiwa kwenye Ofisi za Mwakilishi wa kudumu wa Swaziland kwenye Umoja wa Mataifa. Kunako mwaka 1992 hadi mwaka 1994 akawa katibu wa mwakilishi wa kudumu wa Swaziland kwenye Umoja wa Mataifa, utume ambao aliendelea kuufanya kati ya mwaka 1994 hadi mwaka 1995 kwenye Ubalozi wa Korea ya Kusini.

Kunako mwaka 1995 hadi mwaka 2006 akateuliwa kuwa ni mshauri wa mwakilishi wa kudumu wa Swaziland kwenye Umoja wa Mataifa, New York, Marekani. Kunako mwaka 2006 hadi mwaka 2008 akateuliwa kuwa mkurugenzi  mkuu wa Protokali katika Wizara ya mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa. Kunako mwaka 2008 hadi mwaka 2010 akateuliwa kuwa Balozi wa Swaziland kwenye Umoja wa Mataifa. Mwaka 2010 akateuliwa kuwa Balozi wa Swaziland nchini Ubeligiji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.