2015-05-21 15:07:00

Askari simameni kidete kulinda amani, sheria, demokrasia na haki msingi


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 21 Mei 2015 amekutana na kuzungumza na ndugu na jamaa ya Askari waliopoteza maisha yao wakati wakitoa huduma kwa nchi yao ya Italia. Amewashukuru kwa ushuhuda wa matumaini ya Kikristo yanayowasaidia katika utekelezaji wa dhamana yao kama Askari, huku wakitekeleza wajibu wao katika uaminifu unaolenga mafao ya wengi; ujasiri unaosaidia makuzi ya mtu na jamii inayomzunguka pamoja na kuunza mazingira yanayowawezesha watu kuishi katika uhuru na kwa kuheshimiana

Askari wanapaswa kutoka ili kuonesha tunu msingi katika maisha ya kiraia kwa kujikita katika nidhamu, uwajibikaji na majitoleo ya binafsi kwa ajili ya kulinda amani, sheria za nchi, demokrasia pamoja na kupambana na uhalifu wa magenge pamoja na vitendo vya kigaidi. Hii ni dhamana inayohitaji ujasiri ili kuwaokoa watu ambao wako hatarini pamoja na kuwatia mbaroni wale wanaovunja sheria. Umoja na mshikamano unawasaidia askari kuwa na nidhamu, watu huru dhidi ya watenda maovu wenye nguvu kiuchumi, wala rushwa na mafisadi.

Baba Mtakatifu anawaambia Askari hawa kwamba, kila majitoleo yanayotekelezwa kwa moyo wa upendo na kwa mafao ya wengi, yatapewa tuzo na Mwenyezi Mungu. Huu ni ujumbe mahususi kwa ndugu na jamaa ya Askari ambao wamepoteza maisha yao wakiwa katika huduma kwa nchi yao. Mtu anayetekeleza kazi yake kwa ujasiri na kujihinisha kwa pamoja, atakumbana na matatizo yanayotokana na kazi yake kama njia ya kujisadaka kwani hapa anatembea katika Njia ya Kristo aliyekuja kuhudumia na wala si kuhudumiwa.

Baba Mtakatifu anawaambia ndugu na jamaa ya Askari waliopoteza maisha yao wakati wakitoa huduma kwa Serikali, kwamba, mtu anayetekeleza wajibu wake barabra na kujisadaka kwa ajili ya Jumuiya, hususan kwa wale ambao wako hatarini anapata utimilifu wa maisha yake, hata kama machoni pa wengi ataonekana kuwa amefariki dunia, kama ilivyokuwa kwa Yesu mwenyewe, aliyeteswa, akafa na hatimaye akafufuka kwa wafu.

Tafakari ya kina kuhusu Yesu msalabani inaweza kuwapatia nguvu ya kusamehe na faraja na kwamba, misalaba na mahangaiko yao, yataweza kukombolewa kwa njia ya Msalaba wake, kumbe kila shida na mahangaiko ya mwanadamu yapata kutoka kwa Yesu, malipo na ukombozi. Huu ni mwaliko wa kuendelea kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo katika uhalisia wa maisha. Kazi ya Askari Polisi inahitaji umakini na udumifu ili kuhakikisha kwamba, sheria inatekelezwa, amani na usalama vinadumishwa kwa ajili ya wengi.

Baba Mtakatifu kwa moyo wa shukrani amewakumbuka Askari ambao wanaendelea kuwa mstari wa mbele kwa kutoa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta nafuu ya maisha nchini Italia pamoja na kupambana na watu wanaofanya biashara haramu ya binadamu. Katika matukio yote haya, kama Askari watambue kwamba, wanatekeleza dhamana hii kwa ajili ya huduma kwa binadamu, kabla ya kuanza kufikiria kuhusu kanuni na sheria. Hii ni dhamana ya kimaadili inayowasukuma kutenda mema, ili kuokoa maisha ya watu.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Askari kujivunia kazi yao, kwa kuhudumia umma pamoja na kuwasaidia watu ambao wako hatarini, kwani watakuwa kweli ni mfano mbele ya jamii inayowaona wakitoa huduma endelevu kwa moyo wa ukarimu bila kutafuta mafao yao binafsi. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaweka ndugu, jamaa na askari wa Jeshi la Polisi chini ya usimamizi na ulinzi wa Bikira Maria na Malaika mkuu Mikaeli, ili wawalinde na kuwasaidia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.