2015-05-20 15:44:00

Msiogope kutangaza wala kushuhudia Habari Njema ya wokovu kwa Walimwengu


Wakristo wanapaswa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu pasi na woga wala makunyanzi kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhusika mkuu katika mchakato wa Uinjilishaji. Ikumbukwe kwamba, Kanisa lina asili mbili: ile ya Kimungu kwa sababu limeanzishwa na Yesu Kristo mwenyewe, ambaye ndiye kichwa cha Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa. Waamini wanapaswa kuungana na Yesu ili kutekeleza dhamana ya Uinjilishaji kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji.

Siku ile ya Pentekoste Roho Mtakatifu, aliwashukia wanafunzi na kukaa nao milele, akasaidia mchakato wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kati ya Mataifa. Roho Mtakatifu katika nyakati zote hulifanya Kanisa kuwa moja katika ushirika na huduma na kulifadhili vipawa na karama mbali mbali. Kanisa limepitia katika mitikisiko mingi, lakini bado linaendelea na dhamana ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kumbe hakuna sababu ya waamini kuogopa kutangaza na kushuhudia kwa imani na matendo Habari Njema ya Wokovu.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambaba Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambaye pia ni Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea amani na kuwaaga wanafunzi Wakatoliki kutoka Tanzania ambao wanahitimu masomo yao kwa mwaka 2015. Hii ilikuwa pia ni Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni, tarehe 17 Mei 2015.

Askofu mkuu Rugambwa anasema kwamba, waamini wanaimarishwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu ili kutekeleza dhamana na wajibu wao katika maisha na utume wa Kanisa. Ni dhamana yao kuhakikisha kwamba, wanatumia kila fursa inayopatikana iliĀ  kujichotea ujuzi, maarifa na mbinu za kutangaza Injili kwa watu wa nyakati hizi, lakini kamwe, wasiogope kwani Roho Mtakatifu anaendelea kutenda kazi ndani ya Kanisa, licha ya mapungufu na madhaifu ambayo wakati mwingine yanajitokeza kwa Watoto wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.