2015-05-20 14:27:00

Injili ya Familia: Dhamana ya familia katika malezi ya watoto wao!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 20 Mei 2015 ameendelea kutafakari Injili ya Familia kwa kujikita katika dhamana ya familia katika mchakato wa kutoa malezi kwa watoto, ili waweze kukua na kukomaa kwa ajili yao binafsi na wengine. Kanisa linatambua matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo wazazi na walezi katika utekelezaji wa dhamana hii nyeti, lakini haliĀ  ni mbaya zaidi kwa watoto wanaoishi kwenye familia ambamo wazazi wametengana.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, malezi makini ni uti wa mgongo kwa ajili ya jamii ambayo ni safi. Utume wa malezi ni muhimu na nyeti kutokana na ukweli kwamba, leo hii familia nyingi zinakabiliana na changamoto na matatizo mengi. Kutokana na pilika pilika za maisha, wazazi wanajikuta hawana muda mwingi wa kukaa na watoto wao na kwamba, shule zimechukua nafasi kubwa katika majiundo ya watoto: kufikiri pamoja na kuwarithisha tunu msingi za maisha.

Baba Mtakatifu anakazia kusema kwamba, kuna haja kwa familia na shule kuwa na mahusiano yenye uwiano mzuri. Watoto wanahitaji mwongozo bora katika mchakato wa makuzi na malezi yao, ili waweze kuwajibika kwa ajili yao wenyewe na kwa ajili ya wengine. Jumuiya za Kikristo zinahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, zinasaidia majiundo ya watoto, dhamana inayotekelezwa na familia. Dhamana hii itekelezwe kwa kuwa waaminifu kwa Neno la Mungu, ili kukuza na kudumisha imani, mapendo na uvumilivu.

Baba Mtakatifu Francisko anakumbusha kwamba, hata Yesu mwenyewe alipata malezi na makuzi yake kutoka katika Familia Takatifu, ndiyo maana anathubutu kusema, ndugu zake ni wale wote wanaosikiliza na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha yao. Yesu anawakumbusha wafuasi wake kwamba, mapungufu na madhaifu yao na familia yanaweza kupata neema na baraka kutoka kwake, ikiwa kama watamkimbilia, lakini dhamana ya elimu na malezi kwa watoto ni muhimu sana kwa familia.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuendeleza Injili ya Familia kwa kukabiliana n achangamoto za maisha pasi na kukata tamaa, daima wakimbilie katika tunza na ulinzi wa Bikira Maria. Roho Mtakatifu mfariji, awaimarishe katika mchakato wa malezi kwa watoto wao. Wazazi wawe ni mfano bora wa kuigwa kwa watoto wao katika hekima, kimo na neema, ili kumpendeza Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, tarehe 24 Mei 2015, Familia ya Mungu nchini China itasali kumwomba Bikira Maria wa Sheshan wa Shanghai, ili awaonjeshe upendo na huruma inayobubujika kutoka kwa Kristo. Huu ni mwaliko anasema Baba Mtakatifu, kwa Kanisa zima kuwasaidia Wakristo nchini China, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda amini kwa upendo na huruma ya Mungu kati ya ndugu zao; daima wakiwa wameungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro, mwamba ambao Yesu amejenga Kanisa lake.

Baba Mtakatifu Francisko amekumbusha pia kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, Jumamosi ijayo, katika kesha la Pentekoste, watasali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Wakristo wanaouwawa, kuteswa na kunyanyasika sehemu mbali mbali za dunia, kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Baba Mtakatifu anapenda kukazia umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kudumisha uhuru wa kuabudu, haki msingi ya binadamu ambayo haina mbadala. Jumuiya ya Kimataifa isaidie kusitisha mauaji ya Wakristo yanayoendelea kutendeka kwa nyakati hizi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.