2015-05-19 08:38:00

Vyanzo vya njaa na utapiamlo: Ukata & athari za mabadiliko ya tabianchi


Wajumbe waliokuwa wanashiriki katika mkutano mkuu wa XX wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, Jumanne tarehe 19 Mei 2015 wameshiriki katika maadhimisho ya Siku ya Caritas kwenye onesho la kimataifa la Chakula, Expo Milano 2015. Viongozi wakuu wa Caritas, katika siku hii wamebainisha tafiti zinazoonesha mambo msingi yanayochangia kuongezeka kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha duniani. Kati ya mambo haya ni ukata wa rasilimali fedha; uzalishaji duni wa mazao ya chakula pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kuwatumbukiza mamillioni ya watu katika umaskini na baa la njaa.

Tukio hili la pekee ni sehemu ya maadhimisho ya mkutano mkuu wa XX wa Caritas Internationalis. Kardinali Oscar Rodriguez Maradiaga, Rais wa Caritas aliyemaliza muda wake wa uongozi akiwa ameandamana na Kardinali Luis Antonio Tagle, Rais mpya wa Caritas Internationalis, wamefafanua kwa kina na mapana changamoto hizi katika mchakato wa mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo wa kutisha miongoni mwa watoto.

Caritas inasema kwamba, ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula duniani ni matokeo ya ukosefu wa rasilimali fedha na ardhi; pembejeo za kilimo; mikopo na masoko ya uhakika wa mazao yanayozalishwa hasa kutoka kwa wakulima wadogo wadogo. Bado uzalishaji wa mazao ya chakula uko katika kiwango kidogo sana, kiasi kwamba tija yake hairidhishi hata kidogo.  

Dr. Michel Roy, Katibu mkuu wa Caritas Internationalis anabainisha kwamba, changamoto kubwa kwa sasa ni athari za mabadiliko ya tabianchi; mambo ambayo yanaendelea kuwatumbukiza maskini katika umaskini zaidi. Hapa Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwekeza zaidi katika uzalishaji wa mazao ya chakula ili kuweza kuwa na uhakika wa usalama wa chakula duniani.

Dr. Carolyn Woo, Rais wa Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki, CRS anasema kwamba, utafiti huu unaonesha mchakato wa mahangaiko ya wakulima wadogo wadogo wanaoteseka ili kuhakikisha kwamba, chakula kinapatikana kwa walaji walau kwa kipindi cha mwaka mzima, lakini athari za mabadiliko ya tabianchi yanawafanya wakulima wengi kushindwa kutekeleza dhamana hii nyeti. Inakadiriwa kwamba, asilimia 19% ya wajumbe wa Caritas wanasema kwamba, nchi zao zinaweza kuzalisha chakula cha kutosha pamoja na kupata chakula cha ziada. Lakini sehemu kubwa ya wajumbe wanasema kwamba, nchi zao hazina uhakika wa usalama wa chakula .

Ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula ni matokeo pia uwepo wa makundi makubwa ya wahamiaji wanaotafuta usalama wa maisha yao: kuna pengo kubwa la kipato kati ya jamii ya watu; kuna baadhi ya watu wanakula na kusaza, lakini makundi makubwa ni wale “Akina yakhe, pangu pakavu tia mchuzi” bila kusahau uhalifu, vita na kinzani za kijamii zinazopelekea wakulima kushindwa kutekeleza wajibu wao barabara. Ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula unachangia kuporomoka kwa afya za wengi; ongezeko la vifo hususan watoto wadogo na madhara yake yanajionesha kwa namna ya pekee katika masuala ya elimu, ongezeko la rushwa na ufisadi pamoja na utegemezi mkubwa wa chakula.

Watu wengi wanaaamini kwamba, ikiwa kama sekta ya kilimo itaboreshwa, kuna uwezekano mkubwa wa kuwa na uhakika wa usalama wa chakula duniani. Baadhi yao wanadhani kwamba, mabadiliko ya sera na mikakati ya kilimo, yanaweza kuchangia tija na ufanisi katika masuala ya kilimo na kwamba, kuna haja ya kuwa na mikakati itakayowanufaisha wakulima wadogo wadogo.

Caritas amekuwa ni mdau mkubwa wa maendeleo endelevu ya binadamu na kwamba, huduma zake zimewafaidia watu zaidi ya millioni 106 katika kipindi cha mwaka 2013. Mafunzo kwa wakulima wadogo wadogo yalipewa kipaumbele cha kwanza na kufuatiwa na kilimo endelevu; ugavi wa chakula cha msaada pamoja na maboresho ya mchakato wa lishe na afya.

Caritas inabanisha kwamba, nchi zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara zimeathirika vibaya zaidi kutokana ukosefu wa tija na athari za mabadiliko ya tabianchi; Bara la Asia wao wanaathirika kutokana na ukweli kwamba, wakulima wadogo wadogo hawana uwezo wala nguvu ya kiuchumi kiasi cha kupewa mikopo pamoja na ukosefu wa utawala bora. Nchi za Amerika ya Kusini na Caribbeani zimeathirika zaidi kutokana na mfumuko wa bei za mazao ya chakula pamoja na ukosefu wa miundo mbinu ya usafirishaji. Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini, wao wanaathirika zaidi na vita pamoja na migogoro ya kisiasa na kijamii pamoja na ukosefu wa maji safi na salama.

Itakumbukwa kwamba, Caritas Internationalis ni Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa linalotekeleza dhamana na wajibu huu nyeti katika nchi 200. Utafiti huu umefanywa na Caritas pamoja na wadau wengine. Nchi 99 kati ya nchi 160 zimeshiriki kikamilifu katika utafiti huu. Ni matumaini ya Caritas kwamba, kwa njia ya mshikamano wa dhati, baa la njaa na utapiamlo linaweza kupewa kisogo na Jumuiya ya Kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.