2015-05-19 15:32:00

Jifunzeni kuonja mateso na mahangaiko ya watu wakati wa kuagana!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 19 Mei 2015 amewataka waamini kufanya tafakari ya kina, siku ile watakapokuwa wanafunga vilago vya maisha yao hapa duniani, kama Yesu alivyokuwa anawaaga wafuasi wake siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, kama alivyofanya Mtume Paulo kabla ya kuondoka kutoka Mileto kuelekea Yerusalemu. Baba Mtakatifu amewakumbuka wakimbizi na wahamiaji wanaolazimika kukimbia nchi zao kutokana na dhuluma na nyanyaso kama inavyotokea huko Myanmar, Wakristo huko Mashariki ya Katia au Wayazid kutoka Iraq.

Yesu aliwaaga wafuasi wake akwaahidia kuwapelekea Roho Mtakatifu atakayewafundisha na kuwakumbusha yote aliyowafundisha. Mtume Paulo anawaaga ndugu zake katika Kristo kwa machozi, kwa kuonesha uchungu uliokuwa moyoni mwake kuagana na watu ambao walipendana na kushibana katika Kristo. Kuna watu wanaoteseka baharini na kwenye jangwa, wanapofaulu kufika katika mji fulani wanapatiwa maji na chakula na baadaye wanalazimishwa kuendelea na safari isiyokuwa na ukomo.

Yote haya ni matukio ya kibinadamu yanayoonesha jinsi ambavyo watu wanaagana, kwa mama kumkumbatia mtoto wake anayekwenda vitani, na kila wakati moyo wake unateseka, lakini hakuna hata siku moja, ambayo atakutana na kiongozi wa Jeshi atakayekwenda kumwambia, asante sana Mama kwa sadaka ya mtoto wako kwa ajili ya ulinzi na  usalama wa nchi yake. Waamini wajifunze kujiandaa kuanza safari ya maisha ya uzima wa milele.

Matukio ya kuagana yanaonesha matumaini ya kuonana tena panapo majaliwa! Kwa mtu ambaye hana tena matumaini ya kukutana na ndugu zake, hapa kuagana kunaacha chapa ya majonzi, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo, lakini anajiaminisha kwa Mwenyezi Mungu, ndiyo maana hata Yesu katika sala yake ya Kikuhani anawaweka wafuasi wake chini ya ulinzi na tunza ya Baba yake wa mbinguni.

Waamini wajiandae kukabiliana na Fumbo la Kifo kwa imani na matumaini. Wafikirie na kutafakari yale ambayo wanaacha nyuma yao; Je, wako tayari kuwaacha ndugu na jamaa zao chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu? Liturujia ya Neno la Mungu, iwe ni fursa ya kutafakari na kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya maisha ya uzima wa milele, kwa kujiachilia mikononi mwa Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.