2015-05-19 15:10:00

Askofu mkuu Protase Rugambwa asema: Uinjilishaji bado ni shughuli pevu!


Kanisa ni Sakramenti ya wokovu kwa watu wote, linatumwa ulimwenguni kushuhudia na kutangaza  habari Njema ya Wokovu sanjari na ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaojikita katika misingi ya haki, amani, utulivu, maridhiano, ustawi na maendeleo ya wengi. Ikumbukwe kwamba, Uinjilishaji ni dhamana inayopaswa kutekelezwa na Wakristo wote na wala si Wakleri au watawa ambao kimsingi ni mihimili ya Uinjilishaji. Kanisa linahimizwa kuendeleza dhamana ya Uinjilishaji kwa Watu wa Mataifa, kwa kushirikiana na Roho Mtakatifu.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambaye pia ni Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa, wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu, Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni, sanjari na kuombea amani na utulivu nchini Tanzania pamoja na kuwaaga wanafunzi Wakatoliki kutoka Tanzania wanaohitimu masomo kwa mwaka 2015.

Anasema Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walichapisha hati maalum kuhusu Kazi za Kimissionari za Kanisa, maarufu kama Ad Gentes. Kuna mengi ambayo yamefanyika katika mchakato wa Uinjilishaji Barani Afrika, lakini dhamana hii bado ni pevu sana, kutokana na taarifa zinazoletwa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka Barani Afrika.

Uinjilishaji ni dhamana ambayo inapaswa kumwilishwa katika matendo yanayogusa undani wa mtu kama sehemu ya ushuhuda wa maisha na upendo wa Kikristo katika majadiliano ya kina. Huu ni mwaliko wa kuhakikisha kwamba, Kanisa linaendelea kujielekeza katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaomsikiwa katika misingi ya: haki, amani, upendo na mshikamano wa kidugu. Hii ni changamoto pevu inayowataka Wakristo kumwilisha fadhila za Kikristo katika uhalisia wa maisha na utume wao, ili kweli Ufalme wa Mungu uweze kuenea sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.