2015-05-18 15:10:00

Wanawake walionyanyasika kijinsia nchini DRC waanza kupatiwa tiba makini


Kikundi cha Madaktari wasiokuwa na mipaka, kimekuwa kikitoa huduma za matibabu kwa wanawake na wasichana ambao wamebakwa na kunyanyaswa kijinsia nchini DRC, kutokana na vita inayoendelea nchini humo. Wanawake kutoka eneo la Kikamba, ndio walioathirika zaidi. Huduma hii kwa wanawake, imekuwa ikitolewa kwa kujali utu na heshima yao. Haya ni mateso makali na udhalilishaji wa heshima ya wanawake kutokana na mashambulizi yanayofanywa na majeshi ya waasi nchini DRC.

Wanajeshi hao pia wanawateka watoto nyara na kuwalazimisha kubeba mizigo ya wizi na baadaye kuwaachilia huru. Mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na wanajeshi waasi yamepelekea watu kukimbilia msituni kwa kuhofia usalama wa maisha yao. Kutokana na huduma makini inayotolewa na Kikundi cha Madaktari wasiokuwa na mipaka, wanawake wengi wameanza kujitokeza ili kupatia tiba baada ya kubakwa na kunyanyaswa kijinsia. Hawa ni wasichana na wanawake wenye umri kati ya miaka 14 hadi 70.

Taarifa inabainisha kwamba, wanawake wengi waliotendewa unyama huu wanahofia kutoa taarifa kwa kulinda utu na heshima yao mbele ya jamii inayowazunguka. Lakini Madaktari wasiokuwa na mipaka wanaendelea kuwahimiza ili waweze kujitokeza kwa kusema ukweli na hatimaye, kupata tiba. Madaktari hawa tangu kunako mwaka 2010 wamekuwa wakitoa huduma katika Kituo cha Afya cha Kikamba, eneo ambalo kuna idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.