2015-05-18 07:24:00

Vipaumbele vya Caritas: mafao ya binadamu, utu na heshima yake!


Wajumbe wa mkutano mkuu wa XX wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis wamehitimisha mkutano kwa kumchagua Kardinali Luis Antonio Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila, Ufilippini kuwa Rais mpya wa Caritas. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika Ibada ya misa takatifu kwa ajili ya wajumbe hawa, amewataka kuhakikisha kwamba, Caritas inatoa kipaumbele cha pekee kwa mafao ya binadamu, lakini zaidi kwa wale wanaoteseka na kusukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kardinali Parolin amewakumbusha wajumbe kwamba, hakuna huduma ya upendo inayotolewa na Caritas isiyokuwa na uhusiano na muungano wa dhati na Mama Kanisa anayetambua kwamba, huduma ya upendo ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wake hapa uniani. Hapa Caritas haina budi kujiwekea mikakati ya maendeleo na utekelezaji wake na wala haina sababu ya msingi ya kushikakama na na mashirika ya fedha ya kimataifa na kitaifa.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Caritas inatekeleza dhamana na wajibu wake mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Caritas ni kielelezo na utambulisho wa huduma ya upendo inayotolewa na Mama Kanisa kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Haya yamefafanuliwa kwa kina na mapana na Kardinali Oscar Rodriguez Maradiaga, Rais mstaafu wa Caritas Internatinalis katika mahojiano maalum na Radio Vatican.

Anasema, mkutano mkuu wa XX wa Caritas umemteua Mwenyeheri mtarajiwa Oscar Romero kuwa ni mtakatifu msimamizi na mwombezi wa Mashirika ya misaada na huduma zinazotolewa na Mama Kanisa. Wanamwomba Mwenyeheri Mama Theresa wa Calcutta pamoja na Mtakatifu Martin De Porres kuwasindikiza katika huduma kwa maskini na wahitaji zaidi.

Kwa namna ya pekee, Caritas inamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuliwezesha kutekeleza dhamana na utume wake miongoni mwa maskini na watu wanaoteseka kutokana na majanga mbali mbali ya maisha. Katika maaisha na utume wake kama Rais wa Caritas, Kardinali Maradiaga anabainisha kwamba, ameweza kutembelea sehemu mbali mbali za dunia na kushuhudia jinsi ambayo Kanisa lilikuwa linajitahidi kumwilisha huduma ya upendo miongoni mwa Familia ya Mungu.

Ni matumaini yake kwamba, Caritas itaendelea kukua na kukomaa kwa kujisimika katika huduma makini kwa maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa jamii, kwa kushirikiana vyema zaidi na Majimbo pamoja na Parokia zinazosimamiwa na kuongozwa na Kanisa Katoliki. Caritas inakabiliwa na changamoto mbali mbali katika maisha na utume wake.

Mosi vita inayoendelea huko Mashariki ya Kati, machafuko na kinzani mbali mbalini mambo ambayo yanahatarisha amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Hii inatokana na ukweli kwamba, biashara haramu ya silaha inaendelea kuwa ni chimbuko la majanga kwa mataifa mengi. Kuna wafanyabiashara wanaoendelea kujitajirisha kwa biashara haramu ya silaha, inayonuka damu ya watu wasiokuwa na hatia. Hii ni kashfa kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Pili kuna wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka katika maeneo ya vita, njaa na umaskini, linalotafuta nafuu na ubora wa maisha Barani Ulaya. Kundi hili kwa masikito makubwa licha ya matatizo na changamoto linalokabiliana nazo, linakumbana pia na sera za ubaguzi wa rangi, kiasi cha kunyanyasa utu na heshima yao na kusahau kwamba, hata wakimbizi na wahamiaji hawa wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Hapa walimwengu wanapaswa kutubu na kumwongokea Mungu, kwani tabia hii ni chukizo mbele ya Mwenyezi Mungu. Dhana ya watu kukimbia nchi zao si ugonjwa bali ni mchakato wa maisha ya mwanadamu. Caritas Internationalis itaendelea kufanya mageuzi katika maisha na utume wake kadiri ya maagizo yanayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, kwa kujikita katika huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu. Ni matumaini ya Kardinali Maradiaga kwamba, Caritas Internationalis itaendelea kuwahudumia watu kwa upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.