2015-05-18 07:10:00

Mwaka wa Watawa: Yaliyojiri katika mkutano kati ya Papa na Watawa Roma


Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani katika ngazi ya Jimbo kuu la Roma, hivi karibuni amekutana na kuzungumza na watawa wa Mashirika mbali mbali yanayotekeleza dhamana na utume wao Jimboni Roma. Ilikuwa ni siku maalum kwa ajili ya kusali, kutafakari na kushirikishana uzoefu na mng’amuzi ya maisha na utume wa watawa ndani ya Kanisa na hatimaye, kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, aliyejibu kwa kina na mapana maswali makuu manne yaliyogusia maisha na changamoto wanazokabiliana nazo watawa katika ulimwengu mamboleo.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anawataka wawat kuhakikisha kwamba, wanakuwa wakweli na waaminifu mbele ya Mwenyezi Mungu na Kanisa lake. Wawe ni mashuhuda wa wito kwa kuendelea kujikita kumtafuta Mungu kwa njia ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni wa jamii. Watawa wa ndani wafungue mioyo na masikio yao ili kusikiliza kilio cha watu wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia. Waone, wasome na kusikiliza juu ya vita, magonjwa na mahangaiko ya watu, tayari kumkimbilia Mungu kwa njia ya sala na huduma makini. Watawa wasijitenge na ulimwengu, lakini wakumbuke daima kwamba, wao si wa ulimwengu huu.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka watawa kuishi kadiri ya sheria, kanuni na taratibu zao, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati. Wito wa maisha na utume wa kitawa ni mapambano endelevu ya maisha ya kiroho. Watoe huduma kwa furaha na upendo wa dhati. Watambue kwamba, wasipokuwa makini, watajikuta wanageuza Jumuiya zao za kitawa kuwa ni “shule ya husuda, majungu, mapambano na misigano” kama inavyojitokeza katika familia na jamii katika ujumla wake.

Rushwa na ufisadi wa mali ya Kanisa vinaweza kujipenyeza hata katika maisha na utume wa watawa, wasipokuwa makini katika uaminifu wao kwa Mungu na Kanisa pamoja na kuhakikisha kwamba, wanamwilisha karama za Mashirika yao kwa kusoma alama za nyakati. Watawa wawe ni watu wenye kumbu kumbu hai, kwa kuonesha shukrani kwa yale yaliyopita tayari kukumbatia ya mbeleni pasi na woga. Watawa waoneshe moyo wa shukrani na mapendo kwa njia ya huduma makini. Maisha ya watawa wa ndani yaendelee kujitajirisha katika sala, tafakari ya Neno la Mungu pamoja na maisha ya Kisakramenti.

Baba Mtakatifu Francisko akizungumzia kuhusu upendo na uaminifu kwa maisha ya kitawa anawakumbusha watawa kwamba, wao ni wachumba wapendwa wa Kristo, wanaojisadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Wao ni kielelezo cha upendo wa Bikira Maria kwa Kristo na Kanisa lake. Huu ni upendo unaomwilishwa katika huduma kwa Mungu na jirani kwa njia ya Kanisa. Lakini kutona na udhaifu wa binadamu, Jumuiya za kitawa wakati mwingine “zinatafunwa na wivu usiokuwa na mashiko wala mvuto; majungu na fitina”.

Watawa wanakumbushwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kuishi katika ukweli, samaha na upatanisho, huku wakisahihishana katika upendo unaopata chimbuko lake katika maisha ya sala na tafakari ya kina. Watawa wajitahidi kumwilisha katika maisha na utume wao, Heri za Mlimani ambazo ni muhtasari wa mafundisha makuu ya Yesu kwa wafuasi wake, chemchemi ya maisha ya sala na utakatifu wa maisha. Kukosa na kukoseana ni sehemu ya maisha ya binadamu, kusamehe na kusahau ni mwanzo wa utakatifu wa maisha anasema Baba Mtakatifu Francisko kwa watawa. Umama wa watawa unaoshuhudiwa ndani ya Kanisa unamwilishwa kadiri ya Injili ya Kristo.

Baba Mtakatifu Francisko akizungumza na watawa kutoka Jimbo kuu la Roma amewakumbusha umuhimu wa Jumuiya za Kitawa kufurahia maisha kwa njia ya sherehe, kwani hizi ni alama za shukrani, chemchemi ya sala, toba, upendo na msamaha wa kweli. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yanapaswa kuwa ni kielelezo cha Familia ya Mungu inayosherehekea: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Watawa wafanye sherehe kwa kiasi na kwa unyenyekevu, kama chemchemi ya kujichotea nguvu pamoja na kumshukuru Mungu kwa wema na ukarimu wake.

Akijibu kuhusu malalamiko ya watawa kutohusishwa kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa mahalia, Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu pamoja na Watawa kuwa mikakati inayojikita katika majadiliano na ukweli; kwa kutambua na kuheshimu karama za mashirika; kwa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa Familia ya Mungu katika Kanisa mahalia.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anasema Kanisa linapoadhimisha Jubilee ya miaka 50 ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuna haja ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu mahusiano kati ya Maaskofu mahalia na Watawa, kama ambavyo Mababa wa Sinodi ya Maisha ya Kuwekwa wakfu kunako mwaka 1994 walivyoomba, lakini hadi sasa bado hakuna mabadiliko ya kina yaliyofanyika. Makanisa mahalia yabainishe mikakati ya shughuli za kichungaji na watawa washirikishe karama za mashirika yao katika utekelezaji wa mikakati ya kichungaji ya Makanisa mahalia. Jumuiya za kitawa zijitahidi kuadhimisha Siku kuu kama kielelezo cha moyo wa shukrani.

Baba Mtakatifu Francisko amepembua kwa kina mapana kuhusu Nadhiri ya Utii kwa kumwonesha Kristo aliyejinyenyekesha akawa mtii, hata kufa Msalabani. Maisha yote ya Kristo yanajikita katika utii kwa Baba yake wa mbinguni, utii wenye baraka na kwamba, utii kwa mtawa ni utume unaojikita katika kumfuasa Yesu kwa karibu zaidi kwa kutambua kwamba, maisha ya kuwekwa wakfu ni zawadi kubwa kwa Kanisa, ingawa wakati mwingine zawadi hii kama Shirika au kama mtawa binafsi, haithaminiwi na wengi.

Mwenyezi Mungu amelipatia Kanisa Mashirika mbali mbali ya kitawa yenye karama ambazo ni utajiri mkubwa kwa maisha na utume wa Kanisa. Watawa wasaidiwe katika kutambua karama za mashirika yao pamoja na kusoma alama za nyakati. Wawe na viongozi wa maisha ya kiroho kutoka ndani au nje ya Shirika husika kwani hii si huduma inayopaswa kutolewa na Wakleri peke yao. Kuna watawa na waamini walei ambao wana busara na hekima, wanaweza kusaidia katika maongozi ya maisha yakiroho kwa watawa. Watawa wanahitaji Mapadre kwa ajili ya kuwaungamisha ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu, lakini wanaweza kupata huduma ya ushauri wa kiroho kutoka kwa watu mbali mbali si lazima wawe ni Mapadre peke yao. Sayansi na wataalam mbali mbali wawasaidie watawa katika malezi na makuzi yao: kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu Francisko anakumbusha kwamba, sehemu kubwa ya watawa ndani ya Kanisa ni watawa wa kike, ambao ni takribani asilimia 80% ya watawa wote ndani ya Kanisa. Watawa wanapaswa kuwa ni uso wa Kanisa na Bikira Maria; tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma makini katika sekta ya elimu, afya na huduma za kijamii. Kanisa bado linachangamotishwa kuhakikisha kwamba, linatoa nafasi na dhamana kubwa zaidi kwa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa.

Kwa mara ya kwanza katika historia anasema Baba Mtakatifu Francisko, Chuo kikuu cha Kipapa cha Antonianum kilichoko mjini kinaongozwa na Mtawa wa kike, maajabu ya Mungu. Baba Mtakatifu amewapongeza na kuwashukuru watawa wagonjwa na wazee ambao wamejisadaka maisha yao yote kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Maisha ya kitawa yana furaha na changamoto zake zinazopaswa kuchukuliwa kwa imani na matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.