2015-05-18 09:42:00

Hija ya kitume nchini Cuba: Kauli mbiu "Mmissionari wa huruma ya Mungu"


Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kufanya hija ya kichungaji nchini Cuba kuanzia tarehe 19 hadi 22 Septemba 2015. Baraza la Maaskofu Katoliki Cuba linabainisha kwamba, hija hii inaongozwa na kauli mbiu “ Mmissionari wa huruma ya Mungu”. Huu ni mwendelezo wa kauli mbiu ambazo zimekuwa ni dira na mwongozo wa Mababa Watakatifu waliotembelea nchini Cuba kwa nyakati tofauti.

Mjumbe wa matumaini na ukweli, ndiyo kauli mbiu iliyooongoza hija ya kichungaji ya Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1989. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI hija yake nchini Cuba kunako mwaka 2012 iliyoongozwa na kauli mbiu “Hujaji wa upendo”. Familia ya Mungu nchini Cuba inapenda kutumia hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, utakaozinduliwa mwezi Desemba 2015.

Maaskofu wanapenda kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuisaidia Familia ya Mungu nchini Cuba kuwa kweli ni Wamissionari wa huruma ya Mungu kama Baba Mtakatifu Francisko anavyojitahidi kushuhudia na kufundisha. Baba Mtakatifu atafanya hija hii ya kitume, akiwa njiani kuelekea nchini Marekani katika maadhimisho ya Siku ya Nane ya Familia Kimataifa, itakayoadhimishwa kwenye Jimbo kuu la Philadelphia, Marekani. 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.