2015-05-16 09:10:00

Familia ni dira na chachu ya maendeleo endelevu ya binadamu!


Familia na maendeleo endelevu ndiyo kauli mbiu iliyoongoza kongamano la kimataifa lililoandaliwa hivi karibuni na Askofu mkuu Bernadito Auza, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la familia pamoja na shirikisho la ustaarabu wa watu la Umoja wa Mataifa. Utu na heshima ya binadamu; ustawi na maendeleo ya wengi; utunzaji bora wa mazingira na mshikamano wa kimataifa ni mambo msingi yaliyopewa kipaumbele cha pekee na Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la familia.

Katika hotuba yake ya utangulizi, Askofu mkuu Auza amekumbushia kwamba, familia ni nguzo msingi katika ustawi na maendeleo ya mwanadamu: kiutu na kijamii, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwekeza zaidi na zaidi katika tunu msingi za maisha ya kifamilia, kama ilivyojitokeza mwaka 2014 alipoitisha kongamano la familia na kuhudhuriwa pia na Bwana Ban Ki-Moon, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa pamoja na viongozi wengine kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa.

Askofu mkuu Vincenzo Paglia anabainisha kwamba,  familia ni kitovu cha maendeleo ya jamii, ndiyo maana hata Malengo ya Maendeleo ya Millenia yanajikita zaidi katika ustawi na maendeleo ya familia ya binadamu. Hapa ni mahali muafaka ambako Jumuiya ya Kimataifa ikifanikiwa kuwekeza zaidi, panaweza kuwa ni mahali muafaka pa maendeleo ya kweli ya mwanadamu.

Mafundisho Jamii ya Kanisa yanatambua na kuthamini utu na heshima ya binadamu, tangu anapotungwa mimba hadi mauti inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu ni mambo ambayo hayana mbadala. Utu wa mwanadamu unahitaji kuendelezwa na kudumishwa kwa njia ya mshikamano unaovuka mipaka ya ubinafsi, upweke hasi unaoweza kuwa ni chanzo cha majanga pamoja na kuwasaidia watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa kuongozwa na kanuni auni, chagua makini kwa mtu binafsi na jamii katika ujumla wake.

Askofu mkuu Paglia anakazia kwamba, utu na heshima ya binadamu ni mambo ambayo yanaichangamotisha Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kupambana na umaskini wa hali na kipato; kufuta ubaguzi ili kujenga usawa sanjari na kudumisha huduma bora za afya na elimu pamoja na kuwajengea wasichana na wanawake uwezo kuchangia katika ustawi na maendeleo ya jamii inayowazunguka.

Ustawi na maendeleo ya binadamu unahitaji uchumi thabiti wenye uwezo wa kusaidia mchakato wa maboresho ya maisha ya watu ndani ya jamii pamoja na kutoa ulinzi na uhakika wa maisha ya sasa na yale ya kizazi kijacho, kwa kukazia haki, amani na maridhiano kati ya watu. Huu ni mfungamano wa kijamii unaosimikwa katika mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa, kikolezo kikuu cha maendeleo endelevu.

Askofu mkuu Pagilia anakazia kwamba, Jamii haina budi kulinda tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwa kuwakinga wanafamilia dhidi ya umaskini ambao unaendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia. Jumuiya ya Kimataifa kwa kuwekeza zaidi katika ustawi na maendeleo ya familia, inaendelea kupanua huduma za elimu, afya na ustawi wa jamii, hata kama kanuni maadili na maisha ya kiroho yanaonekana kupewa kisogo katika mchakato huu wa maendeleo ya binadamu.

Familia ni mahali ambapo kamwe, Jumuiya ya kimataifa haipaswi kubeza. Ndiyo maana, Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la familia amewashukuru na kuwapongeza wanachama wa Shirikisho la ustaarabu wa watu la Umoja wa Mataifa kutokana na mchango wake mkubwa katika mchakato wa majadiliano ya kidini, ili kuboresha mahusiano kati ya watu ili hatimaye, kujenga umoja na mshikamano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.