2015-05-16 14:55:00

Alimwangalia kwa jicho la huruma na mapendo, Mathayo, akachanganyikiwa!


Mpendwa msikilizaji wa kipindi cha hazina yetu, Tumsifu Yesu Kristo. Karibu katika kipindi pendevu cha hazina yetu, tuendelee kuitegea sikio hazina ya Mama Kanisa, ili kutokamo tuweze kuhekimishwa na kukomazwa katika imani, kwa namna ya pekee wakati huu tunapoitikia wito wa Mama Kanisa, ambaye  kwa njia ya waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko, Misericordiae vultus yaani uso wa huruma; anatualika kuimwilisha huruma ya Mungu kwa maneno na matendo ya upendo katika maisha  yetu ya kila siku.

Leo mpendwa msikilizaji tunaendelea na tafakari yetu, ambapo Baba Mtakatifu Fransisko ndani ya “Misericordiae vultus”, anaendelea kutualika kufungua macho ya mioyo na ya mwili, ili Kristo anapotutafuta kwa njia ya neno lake, atupate, anapotutafuta kwa njia ya sakramenti zake atupate. Macho yetu yawe tayari kugongana na macho ya huruma ya Yesu. Jicho la upendo la Yesu lina nguvu ya kupenya na kuingia katika undani kabisa wa maisha yetu na kufanya mabadikilo makali.

Baba Mtakatifu anatutafakarisha neno hilo kwa mwanga wa Injili ya Mathayo 9:9-13/Mk 2:13-17. Kuitwa kwa Matayo, kunaoneshwa katika mwangwi wa huruma. Yesu lipokuwa akipita katika dawati la mtoza ushuru, alimkazia jicho Mathayo. Na haswa, macho ya Mathayo, yaligongana na jicho la huruma la Yesu. Lilikuwa ni jicho, kali, la huruma, lililopenya katika nafsi na maisha mazima ya huyu ndugu mtoza ushuru. Mazingira ya ile meza, ni mazingira ya dhambi. Hivyo haikuwa rahisi kutenganisha kati ya tabia za ile meza na mtu aliyeko pale mezani, kumbe, hakika alikuwa ni mdhambi, mgonjwa wa kiroho na kijamii aliyepaswa kuponywa na Jicho la huruma la Yesu peke yake. (Mk.2:17)

Ni jicho hili kali la huruma, lililoambatana na sauti ya Yesu iliyosema “nifuate”, naye Mathayo akainuka, akamfuata (Mt. 9:9). Jicho la Yesu lililojaa huruma inayochoma mioyo, ni jicho la kimapinduzi. Sauti ya wito ya Yesu, ni amri ya huruma na ya kimapinduzi. Baada ya tazamo ile kuu, tazamo ya kinabii, Matayo hakuhitaji kuuliza ufafanuzi, aliinuka na akamfuata Yesu, huku akifanya mabadiliko ya maisha mazima na kutwaa utume mpya.

Mtakatifu Beda mhashamu kuhusu sehemu hii ya Injili aliandika, “Yesu alimtazama Mathayo kwa huruma ya upendo, na akamchagua “Miserando atque eligendo”, maana yake kuwa na huruma na kuchagua. Kristo Bwana, alimtazama Mathayo kwa huruma, na kisha akamchagua. Pamoja na hali yake mbaya kiroho, baada ya kumtazama kwa jicho la huruma, akamchagua huyo Mathayo kuwa chombo cha kueneza habari njema ya wokovu.

Baba Mtakatifu anasema, maneno haya ya Mtakatifu Beda mhashamu, ndiyo yaliyomwangaza hata akayafanya kuwa ndio Kauli-mbiu yake ya kiaskofu. Mpendwa msikilizaji, Baba Mtakatifu Fransisko anatushirikisha pia undani wa Imani yake juu ya huruma ya Mungu inayomwilishwa kwetu kwa njia ya Kristo Yesu. Katika ile nembo ya Kiaskofu ya Papa Francisko, tunayakuta maneno haya “Miserando atque eligengo”. Ni maneno la Kilatini yenye maana ya kuhurumia ‘miserando’, atque ikimaanisha ‘na’, eligendo ‘kuchagua.’ Papa Francisko anatushirikisha huruma inayotualika kutenda, huruma inayowaelekea wengine ili kuwainua, kuwasaidia, kuwaongoa, kuwafuta vumbi la dhambi katika macho, kuwapelekea uponyaji wa roho na mwili, na kuwasaidia kuuvaa utume mpya, utume mwema katika maisha.

Kwa mantiki nyingine Baba Mtakatifu Francisko anatufundisha kwamba, huruma haiishii tu kutazama na kusikitika, hapana. Ni huruma inayotualika kutenda zaidi. Ni kwa mantiki hii daima Baba Mtakatifu anatualika kuivaa huruma ile inayowaelekea zaidi wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mathayo kwa maisha yake na kazi yake, alikuwa ni miongoni mwa kada za watu wasiopendwa. Watoza ushuru hawakupendwa sana na watu kutokana na kazi yao. Pengine hawakuwa waaminifu, au walikuwa wanawabana mno watu hadi wanakosa raha. Yesu alifahamu hilo, ndiyo maana alimkazia jicho la huruma na kumchagua. Ni jicho lililokwenda kubomoa bomoa milima ya dhambi katika nafsi ya Mathayo na kusafisha kabisa vifusi vya ugumu ya moyo na magonjwa ya Kiroho.

Mpendwa msikilizaji wa kipindi cha hazina yetu, katika maisha yetu sisi sote kuna nyakati tunaketi katika dawati la mtoza ushuru. Pale ambapo tunakosa kutenda haki kwa wenzetu, pale tunaposahau kuishukuru huruma ya Mungu, pale ambapo tunaishi kinyume na mapenzi ya Mungu. Hakika tunakua ni wachukivu kwetu wenyewe na kwa Mungu. Lakini Mungu kwa huruma yake hatukatii tamaa wala hatutupi. Atatuhurumia na kutuchagua. Anatujia katika neno lake na katika Sakramenti, na ni Kristo mwenyewe anatutazama hadi undani kabisa wa mioyo yetu, ili sisi nasi tumtazame, tuchomwe mioyo na tufanye mabadiliko katika maisha yetu.

Mpendwa msikilizaji, kuna wakati ambapo huwa tunageuza shingo ili tusitazamane na Yesu, au tunaziba macho, ili tusilione jicho lake, au tunaziba masikio, tusiisikie sauti yake inayosema nifuate! Ni kwa njia hiyo, ndiyo tunabaki kuogelea katika bwawa la dhambi. Kwa njia ya tendo la Yesu na Mathayo mtoza ushuru, tunajifunza kwamba, sisi kama wanadamu, ili kuweza kufanya mabadiliko kiroho na kimwili, tunahitaji kushirikiana na huruma ya Mungu. Utayari na utii wa Mathayo, ulimfanya abadili kabisa maisha yake. Nasi, kwa utayari na utii wetu kwa huruma ya Kristo tutaokoka.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.