2015-05-15 13:54:00

UN: Dini zina mchango mkubwa katika ustawi na maendeleo ya binadamu!


Bwana Ban Ki-Moon Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa katika ujumbe aliowaandikia washiriki wa mkutano mkuu wa XX wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, anaipongeza Caritas kwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia sanjari na kubainisha mikakati inayopaswa kufanyiwa kazi baada ya mwaka 2015, ili kudumisha utu na heshima ya binadamu.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anabainisha kwamba, maendeleo endelevu na mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi ni mambo ambayo yanaitaka Jumuiya ya Kimataifa kufanya kazi kwa ushirikiano kwa ajili ya mafao ya wengi. Athari za mabadiliko ya tabianchi ni changamoto ya kimataifa kwani wote wanaathirika, ingawa kwa viwango tofauti, mwaliko wa kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inarithisha vijana wa kizazi kipya dunia iliyo safi.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema kwamba, dini zina mchango mkubwa katika utunzaji wa mazingira, lakini kwa bahati mbaya, ni kundi ambalo halisikilizwi, lakini athari zake ni kubwa katika uharibifu wa mtandao wa maisha. Mazingira hayana budi kulindwa na kuendelezwa kwa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, ili kuibua malengo mapya ya maendeleo kwa ajili ya ustawi wa binadamu, kwa kusimama kidete kupambana na baa la njaa duniani sanjari na kuibua vipaumbele vya kiuchumi na kijamii vinavyopaswa kufanyiwa kazi.

Jumuiya ya Kimataifa anasema Bwana Ban Ki-Moon inaweza kufanikiwa kufikia lengo hili kwa kung’oa baa la umaskini, kwa kuondoa utengano wa kijamii na kulinda mazingira kadiri ya mafundisho makuu ya dini. Jumuiya ya Kimataifa inasubiri kusikia sauti yenye nguvu ya kimaadili katika mikutano ya kimataifa inayotarajiwa kufanyika huko Addis Ababa mwezi Julai, kuhusiana na masuala ya fedha na mwezi Septemba, kuhusiana na mikakati ya maendeleo baada ya mwaka 2015 na mwishoni ni mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika nchini Ufaransa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.