2015-05-15 06:51:00

Kard. Luis Antonio Tagle achaguliwa kuwa Rais wa Caritas Internationalis


Wajumbe wa mkutano mkuu wa XX wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, wamemchagua Kardinali Luis Antonio Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila, Ufilippini kuwa Rais mpya wa Caritas Internationalis. Kardinali Tagle anachukua nafasi ya Kardinali Oscar Rodriguez Maradiaga ambaye ameiongoza  Caritas Internationalis kwa awamu mbili mfululizo. Bwana Alexander Bodmann kutoka Austria amechaguliwa kuwa Mweka hazina mpya wa Caritas Internationalis.

Kardinali Tagle mwenye umri wa miaka 57 anakuwa ni Rais wa kwanza wa Caritas kuchaguliwa kutoka Barani Asia. Lakini huyu ni kati ya viongozi wa Kanisa Barani Asia ambaye amejipambanua kwa unyenyekevu pamoja na kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kardinali Tagle amepokea dhamana hii mpya kwa moyo wa unyenyekevu, akisema kwamba, anatambua kuwa ana mapungufu mengi, lakini kwa njia ya mshikamano na wajumbe wote wa Caritas, huku wakisukumwa na upendo wa Yesu uliomiminwa mioyoni mwao na kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, amekubali kupokea dhamana hii.

Kardinali Tagle anawaalika wajumbe wa Caritas kushikamana kwa pamoja ili kuliimaarisha Kanisa la Maskini, ili ushuhuda wao uweze kuleta mvuto katika maelewano, haki, uhuru wa kweli na amani. Wajumbe wa mkutano mkuu wa Caritas Internationalis, kwa pamoja wamempongeza na kumshukuru Kardinali Oscar Rodriguez Maradiaga aliyemaliza muda wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.