2015-05-15 10:39:00

Askari lindeni amani na kudumisha mchakato wa huduma kwa maskini!


Maaskofu wa Majimbo ya Kijeshi Barani Ulaya kuanzia tarehe 11 hadi tarehe 15 Mei 2015 wamekuwa wakishiriki katika kongamano la nne la kimataifa, lililowapatia fursa ya kuangalia utambulisho na utume wa vikosi vya ulinzi na usalama kwa ajili ya kuenzi amani duniani. Kardinali Marc Ouellet, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maaskofu pamoja na viongozi kadhaa wameshiriki na kutoa mada katika kongamano hili.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anakazia umuhimu wa vikosi vya ulinzi na usalama ili kudumisha mchakato wa amani dhidi ya uchu wa baadhi ya watu wanaotaka kusababisha machafuko na vita kwa mafao yao binafsi. Askari wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanaendelea kumwilisha wito wa maisha yao kama Wakristo, kiasi hata cha kuwa tayari kujisadaka maisha kwa ajili ya huduma kwa Mungu na ndugu zao, kama kielelezo cha muungano wao na Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu.

Baba Mtakatifu anawahamasisha askari kukumbatia maisha na huduma hii pamoja na kuendelea kufarijiwa na Mama Kanisa wanapotekeleza dhamana na wajibu wao, kwa kutambua kwamba, mara nyingi wanakabiliwa na kifo machoni pao, kumbe, Kanisa halina budi kuwapatia ujumbe wa imani na matumaini unaofumbatwa katika urafiki, upendo na msamaha.

Kardinali Marc Ouellet anasema kwamba, kuna haja kwa viongozi wa Kanisa kufanya tafakari ya kina kuhusiana na historia na maisha ya Maaskofu wa Majimbo ya kijeshi katika miaka ya hivi karibuni, mintarafu Katiba ya kitume juu ya huduma za maisha ya kiroho kwa wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama. Lengo ni kuhakikisha kwamba, miundo mbinu iliyopo inakidhi mahitaji ya waamini wa Majimbo ya Kijeshi, kwa kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai sanjari na kudumisha amani.

Kanisa linapenda kujielekeza zaidi katika mchakato wa kutafuta, kulinda na kudumisha amani sehemu mbali mbali za dunia; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao na ustawi wa wengi. Haya ni mambo ambayo yanapaswa kupewa msukumo wa pekee na Jumuiya ya Kimataifa. Hapa kuna haja anasema Kardinali Mar Ouellet kuendelea kutangaza Habari Njema ya Wokovu inayofumbatwa katika kanuni maadili na amani ambayo inapaswa kueleweka katika mapana yake na wala si suala la kutosikika kwa mtutu wa bunduki.

Amani mintarafu Maandiko Matakatifu inajielekeza zaidi kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa ajili ya kuwalinda na kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hii ni amani inayopania kujenga na kudumisha dunia inayosimikwa katika misingi ya haki na utu wema. Takwimu zinaonesha kwamba, hadi leo hii kuna Maaskofu 36 wa Majimbo ya Kijeshi, wanaotekeleza dhamana na wajibu wao sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.