2015-05-14 13:26:00

Familia ni chombo makini cha mawasiliano; mahali pa kukutana katika upendo


Familia ni kituo cha kwanza kabisa cha mawasiliano ya kijamii; changamoto kubwa katika maisha na utume wa Familia, kuhakikisha kwamba, kweli familia zinakuwa ni vyombo makini vya mawasiliano. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa mwaka huu, anahimiza umuhimu wa mawasiliano ndani ya familia, kama eneo mahususi la watu kukutana katika upendo.

Hii ndiyo changamoto ambayo imefanyiwa kazi hivi karibuni na Wakurugenzi wa Idara za mawasiliano ya jamii kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria katika semina yao iliyokuwa inafanyika kwenye mji wa Benin. Wajumbe wanasema kwamba, kuna haja kwa Mama Kanisa kuendelea kuwafundisha na kuwahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema Mafundisho jamii ya Kanisa kuhusu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo na Imani inayopaswa kumwilishwa katika ushuhuda wa maisha, tayari kushiriki katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.

Vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Kanisa vinahamasishwa kufahamu vipaumbele vya maisha na utume wa Kanisa, tayari kuwasaidia waamini kuweza kuvifanyia kazi katika utume wao. Inasikitisha kuona kwamba, kuna mafundisho mengi yanayotolewa na Baba Mtakatifu pamoja na viongozi wa Kanisa, lakini hayawafikii walengwa kama inavyokusidiwa. Dhana ya familia katika vyombo vya habari nchini Nigeria inapewa mwelekeo hasi zaidi, changamoto ya kubadili mwelekeo huu ili kuonesha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya mafundisho ya Kanisa na maadili, utamadui na mila njema za Kiafrika. Lengo ni kukuza utakatifu wa familia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jamii.

Wajumbe wa semina hii wanatambua na kukazia dhana ya familia kama chombo makini cha Uinjilishaji na kwamba, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zinakuzwa na kudumishwa, kwa kujikita katika maisha ya Sakramenti, Tafakari ya Neno la Mungu, Maisha ya Sala; Majadiliano katika ukweli na uwazi pamoja na ushuhuda wa Injili ya Familia yenye mvuto na mashiko katika maisha ya watu. Umefika wakati wa kukazia umoja, upendo na mshikamano wa dhati katika maisha ya ndoa na familia, badala ya kubeza na kudhalilisha Injili ya Familia

Wajumbe wanasema, kuna umuhimu kwa Kanisa na Jamii kuendelea kuelimisha umuhimu wa matumizi bora ya mitandao ya kijamii kwa ajili ya ustawi, mshikamano, umoja na maendeleo ya familia. Ikumbukwe kwamba, mitandao ya kijamii, isipotumiwa vyema inaweza kuwa ni chanzo cha kuporomoka kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Mitandao ya kijamii, iwe ni fursa ya kukuza upendo, umoja, amani na mshikamano kwa wanandoa pamoja na familia zao. Kamwe wanandoa wasikubali kuvuruga maisha yao kwa kuwa na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.