2015-05-13 08:48:00

Mwaka wa Watawa Duniani: Papa kukutana na watawa wa Roma, 16 Mei 2015


Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani yanaendelea kutimua vumbi sehemu mbali mbali za dunia kwa njia ya tafakari, sala na makongamano kama sehemu ya mchakato wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ajili ya maisha ya kitawa ndani ya Kanisa. Kardinal Agostino Vallini, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma anasema, kwamba, Jumamosi tarehe 16 Mei 2015, Ukumbi wa Paulo VI utawaka vumbi kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Jimbo kuu la Roma.

Hii itakuwa ni siku ya sala, tafakari na ushuhuda kutoka kwa watawa wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kushirikishana uzoefu na mang’amuzi katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Hivi ndivyo watawa wanavyotarajiwa kujimwaga kwenye Ukumbi wa Paulo VI kama maadhimisho ya Siku ya Watawa Jimbo kuu la Roma, awamu ya kwanza. Awali ya pili, baada ya kardinali Vallini kutoa hotuba ya utangulizi, Baba Mtakatifu Francisko atakuwa tayari kujibu maswali manne yatakayoulizwa kwake na wawakilishi wa watawa kutoka Jimbo kuu la Roma.

Itakumbukwa kwamba, Jimbo kuu la Roma lina watawa ishirini na tano elfu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, hii pia itakuwa ni siku ya watawa hawa kukutana, kuzungumza na kuonesha karama na mapaji ambayo Mwenyezi Mungu amewajalia kwa ajili ya sifa na utukufu wa Kanisa pamoja na huduma kwa mwanadamu. Upendo na ukarimu; katekesi makini na sanaa ni kati ya mambo ambayo yatajadiliwa wakati wa maadhimisho haya. Wengi wa watawa hawa ni wale wanaotekeleza dhamana na utume wao nje ya mji wa Roma, miongoni mwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.