2015-05-13 09:32:00

Kanisa Katoliki Msumbiji: Changamoto za maisha na utume wa Kanisa!


Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji kuanzia tarehe 9 hadi 15 Mei 2015 linafanya hija ya kitume ambayo hufanyika walau kila baada ya miaka mitano. Hii ni nafasi yak usali, kutafakari na kushirikishana na Baba Mtakatifu pamoja na waandamizi wake maisha na utume wa Kanisa mahalia. Kanisa Katoliki nchini Msumbiji linaendelea kustawi na kushamiri, kwa sasa kuna Majimbo kumi na mawili na kwamba, uhusiano kati ya Serikali na Kanisa unaendelea kuboreka siku hadi siku hususan katika huduma za kijamii.

Kunako mwaka 2007 Serikali ya Msumbiji iliamua kurejesha nyumba za Ibada zilizokuwa zimetaifishwa na Serikali kunako mwaka 1977. Mahusiano ya Serikali ya Msumbiji na Vatican yakaboreshwa zaidi kunako mwaka 2011, pande hizi mbili zilipotiliana Mkataba wa ushirikiano katika masuala elimu pamoja na Serikali kutambua kisheria ndoa zinazofungwa na waamini wa Kanisa.

Kunako mwaka 2013, Bwana Alberto Clementino Vaguina, Waziri mkuu wa Msumbiji alikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko kwa pamoja walipongeza mchango wa Kanisa katika mchakato wa kuleta amani, maridhiano, ustawi na maendeleo ya wengi kwa kujikita katika sekta ya elimu, afya na matendo ya huruma.

Msumbiji licha ya kuwa na utajiri wa maliasili na rasilimali nyingi, lakini bado inahesabiwa kuwa ni kati ya nchi maskini sana duniani. Ni nchi ambayo bado inaandamwa na baa la ujinga na magonjwa, mambo ambayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe. Rushwa na ufisadi wa mali ya umma; uhalifu wa magenge, biashara haramu ya dawa za kulevya na binadamu pamoja na kazi za suluba ni kati ya matatizo makubwa yanayoikabili Msumbiji kwa sasa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji linabainisha kwamba, matatizo na changamoto zote hizi ni sehemu ya changamoto na matatizo ambayo Kanisa linapenda kuyapatia kipaumbele cha pekee katika mikakati ya shughuli zake za kichungaji. Hivi ni vikwazo vya maendeleo, lakini pia ni hatari kwa mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na utulivu bila kusahau dhamana ya Kanisa katika Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kuleta athari kubwa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya kwa kutaka kuiga kila jambo wanaloliona kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii; hatari kubwa kwa maisha ya kiroho, maadili na utu wema. Kuna idadi kubwa ya waamini, lakini wale wanaoshiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, hawalingani na idadi ya Wakristo walioandikwa kwenye vitabu vya Ubatizo.

Hapa Kanisa halina budi kuwekeza katika majiundo ya awali na endelevu, ili kuwaimarisha waamini katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kujikita katika maisha ya Kisakramenti pamoja na kushiriki katika vyama vya kitume, mambo msingi yanayosaidia kukoleza na kuimarisha imani ambayo, hatimaye, inamwilishwa katika matendo. Kuna vyama vya kitume vinavyoendelea kuwahamasisha waamini kujikita katika mchakato wa utamadunisho, ili kweli Injili ya Kristo iweze kupenya katika maisha na vipaumbele vya watu. Umoja wa Wanawake Wakatoliki Msumbiji una nguvu sana, ikilinganishwa na vyama vingine vya kitume.

Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji linabainisha kwamba, kati ya vipaumbele vyake vya shughuli za kichungaji ni majiundo makini, utamadunisho wa imani na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Maaskofu wanapenda kuwekeza zaidi katika majiundo kwa waamini walei, ili kweli wasaidie katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mguso.

Utamadunisho wa imani, ni jambo ambalo linaendelea kuvaliwa njuga na Maaskofu kwa kuhakikisha kwamba, waamini wanapewa Katekesi makini kuhusu: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili yanayoongozwa na Amri za Mungu pamoja na Sala, ili kweli Familia za Kikristo nchini Msumbiji, ziweze kuwa ni shule ya sala, vitalu vya miito mitakatifu na chemchemi ya maisha adili na matakatifu, tayari kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji linasema kwamba, ili Kanisa liweze kutekeleza dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza Watu wa Mungu, kuna haja ya kuwa na majiundo bora na makini kwa Wakleri na Watawa kwani hawa ni mihimili mikuu ya Uinjilishaji.

Idadi ya Mapadre bado ni ndogo ikilinganishwa na mahitaji ya Kanisa nchini Msumbiji, kumbe, waamini wanahamasishwa kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea miito mitakatifu, ili kweli Kanisa liweze kupata watendakazi waaminifu, waadilifu, wachapakazi na watakatifu, tayari kujisadaka kwa ajili ya kuwagemea Watu wa Mungu huruma, furaha na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.