2015-05-13 09:42:00

Homilia ya Papa kwa ajili ya ufunguzi wa Mkutano wa Caritas


Baba Mtakatifu Francisko  Jumanne  jioni tarehe 12 Mei 2015  aliongoza Ibada ya Misa kwa  nia ya  kufungua Mkutano Mkuu wa  XX wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki,” Caritas Internationalis”. Ibada hii ilifanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro na ilihudhuriwa na wajumbe wa Mkutano huu Mkuu wa  Caritas Internationalis, kutoka pande zote za dunia. Kati ya Ajenda muhimu za mkutano huu, ni pamoja na  kupitisha Mbinu mkakati wa kufanyia kazi na Bajeti kwa ajili ya miaka minne ijayo.

Baba Mtakatifu Francisko katika  mahubiri yake, alikiri kwamba ,  Utume  wa Caritas , kwa hakika ni ushuhuda wa kweli kwa mafundisho ya Yesu  Kristo . Chombo hiki  Katoliki kwa ajili misaada ya ubinadamu na maendeleo , huonyesha nguvu ya upendo wa Kristo na hamu ya kanisa katika kumfikisha Yesu kwa kila binadamu , na hasa kwa watu maskini na wanaoteseka. 

Baba Mtakatifu alieleza hayo kwa kutafakari  ujumbe wa  somo kutoka  Matendo ya Mitume,  aya zinazoeleza miujiza, iliyowatokea Paulo na Sila walipokuwa wamefungwa  gerezani . Jinsi Bwana alivyowatendea  maajabu, na jinsi mtu anaye sikiliza Neno la Bwana toka kwao, alivyookoka na kuchukua  hatua muhimu, katika  njia  ya kuelekea imani na wokovu.  Mtu  huyo na familia yake , walilisikiliza Neno kutoka kwa  Paulo na Sila , na  maisha yao kubadilika. Mtu huyo aliguswa na mateso ya Paulo na Sila na kuwahudumia kwa upendo mkuu, kuyasafisha madonda na majeraha yao, na  kuwakaribisha nyumbani kwake, na familia nzima kuwa na furaha kamili.

Aidha Baba Mtakatifu alirejea somo la Injili, linalohimiza kuosha miguu na madonda ya wale walio katika mateso na dhiki na kuandaa meza ya chakula kwa ajili yao, akisema hii ni ishara ya unyenyekevu , katika kulikubali Neno na Sakramenti ya ubatizo kwamba daima huandamana na  ukarimu , huduma na kupokea  wengine. Utendaji wote huu umefungamana pamoja  na kuwa na maana moja tu kwamba ni  kumkaribisha Mungu na wengine. Ni  kuwapokea wengine kwa neema ya Mungu; kumkaribisha Mungu kwa kielelezo cha  huduma kwa ndugu zetu wake kwa waume.  Neno, Sakramenti na huduma , inakuwa kwa ajili ya ustawi wa wote , kama shuhuda za tangu mwanzo wa Kanisa zinavyoeleza.

Papa alieleza na kugeukia  utume wa  Caritas, akisema katika kazi zake za  kila siku,  tunaona ishara ya wito mzima wa Caritas. Caritas ambayo kwa sasa ni asasi kubwa yenye kutambuliwa duniani  kote, kutokana na mafanikio ya kazi zake. Papa,  aliitaja huduma ya  Caritas, kuwa ni ukweli wa  Kanisa katika maeneo mengi ya dunia, na hivyo ni lazima iendelee kupanua huduma zake katika Parokia na jumuiya mbalimbali ambako bado kufika. Ni lazima  kupeleka  huduma hii  katika parokia na  jumuiya mbalimbali ambazo bado kufikiwa. Na ni lazima kufanya upya, utendaji wa kanisa, ili iwe  kama ilivyokuwa katika siku zake za mwanzo wa Kanisa.  Papa aliendelea  kufafanua utume wa Caritas kwamba,  kwa kweli, chimbuko la huduma  ya Caritas ni fadhila za kawaida za kumpokea Mungu na jirani kwa utulivu. Na ukarimu huu unapaswa kuanzia ndani ya moyo wa mtu mwenyewe na kutoka kwenda nje, kwenda  kuhudumu wengine katika Jina la Kristo , wote wale wanaokutana nao na wale watakaoendelea kukutana nao na wale watakaowaendea kama majirani. Papa alishukuru kwa hili lakini pia akaonya dhidi ya lengo lake kuu la kuinjilisha  kusahaulika na Caritas  kufanywa kama asasi ya kawaida la misaada ya kibinadamu.

Papa aliendelea kuonya kwamba , kila mhudumu wa  Caritas, si mfanyakazi wa kawaida tu  kama mtoa misaada, lakini anapaswa kuwa shahidi wa kweli wa Kristo. Ni lazima awe  mtu  anayeitafuta sura ya Kristo inayoonekana kwa wateswa na wahitaji ,  na kumruhusu  Kristo kuingia kwake; ni mtu mwenye kuwa na  upendo na roho ya Kristo, roho ya fadhila na tulizo.

 Hivyo Papa akasisitiza , mipango na mikakati yote , ni lazima iandamane na upendo unaochipuka kutoka kwa Kristo mwenyewe , vinginevyo mikakati  na mipango yote ya caritas inakuwa ni mipango tupu isiyokuwa na maana.  Si kutenda kwa upendo wa kibinadamu bali kwa  upendo wake yeye, upendo wa kusafishwa na kuimarisha upendo wa Kristo.

 Kwa namna hiyo Papa alisema , kila mmoja anaweza kumtumikia mwingine , kuandaa meza kwa ajili ya wote, kama Mungu alivyoiandaa meza ya Ekaristi, kwa wote na wakati wote.  Na kufikiri  juu ya  meza ya Ekaristi, tusisahau Wakristo wenzetu, wanaonyimwa haki ya kushiriki katika furaha ya meza hii ya Ekaristi,  kutokana na ghasia  na vita. Pia wale  waliofukuzwa kutoka makazi yao na makanisa yao kuharibiwa . Papa alirudia kukata rufaa  upya ya kutosahaulika watu hao wanaoteswa na udhalimu usioweza vumilika.

Na alikamilisha homilia yake akisema ,Caritas ,  kama ilivyo pia kwa  asasi zingine za fadhila kwa  upendo wa Kanisa, huonyesha  nguvu ya upendo wa Kikristo na hamu ya Kanisa kumfikisha Yesu kwa kila mtu, hasa wakati wale wanaoteswa na umaskini na dhuluma.  Hii ni njia iliyoko mbele ya kila Mkristo. Papa kwa mtazamo huo, alitumaini, ndiyo kazi kubwa kwa kila mmoja kwa siku hizi. Na alikabidhi utendaji wote kwa  kwa Bikira Maria, katika kumkaribisha Mungu na jirani, kama msingi ya maisha Papa  alieleza na kukumbusha kwamba , Jumatano hii 13 Mei ni Siku Kuu ya Mama Yetu wa Fatima, aliyetokea  kutangaza ushindi dhidi ya maovu. Kwa msaada huo mkubwa , hakuna hofu katika kuendelea na  dhamira ya kanisa.  








All the contents on this site are copyrighted ©.