2015-05-12 09:39:00

Tamasha la Muziki Vatican ili kuonesha mshikamano na maskini!


Katika maadhimisho ya Siku kuu ya Kupaa Bwana mbinguni itakayoadhimishwa tarehe 14 Mei 2015 hapa mjini Vatican, kutafanyika tamasha la muziki wa kufa mtu, ambalo limeandaliwa kwa ajili ya maskini na watu wanaoishi katika mazingira magumu hapa mjini Roma. Hawa ndio watakaokuwa wageni rasmi katika tukio hili la aina yake ambalo limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Baraza la Kipapa la utamaduni, Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya, Kitengo cha Sadaka ya Papa pamoja na Mfuko wa Kardinali Van Thuan.

Monsinyo  Diego Giovanni Ravelli, mkuu wa kitengo cha sadaka ya Papa anasema kwamba, tamasha hili la muziki linakuwa ni daraja la wasamaria wema katika kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii: kiroho na kimwili. Tamasha hili litawashirikisha magwiji wa muziki kutoka Jimbo kuu la Roma. Muziki wa kweli ni kielelezo cha upendo kwa Mungu na jirani na kwamba, wimbo mzuri kuliko nyimbo nyingine zote ni ule wa upendo, unaogusa na kutikisa sakafu ya maisha ya mwanadamu kwa njia ya huduma makini.

Monsinyo Ravelli anasema mwanadamu ana kipaji cha kuweza kusikiliza na wala si wote wenye ujuzi na karama ya kuweza kucharaza vyombo vya muziki, kiasi cha kuwaacha wasikilizaji wao wakiwa wamepigwa na butwaa, kwani upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu unagusa wengi na unaweza kufahamika; kwani hii ni lugha inayozungumzwa na wengi.

Wakati wa kuwasilisha maadhimisho ya tamasha hili kwa waandishi wa habari hivi karibuni, viongozi mbali mbali wamechangia mawaso yao na jinsi ambavyo wanataka kulifanikisha tamasha hili na kwamba, fedha yote itakayopatikana itatumika kwa ajili ya huduma ya upendo. Watu watakaoshiriki katika tamasha hili, mwishoni, kila mtu kwa uhuru wake mwenyewe atachangia kadiri ambavyo amekirimiwa na Mwenyezi Mungu katika maisha yake, kwani waswahili wanasema, aliyekupa wewe ndiye aliyeninyima mimi!

Baba Mtakatifu anaendelea kutekeleza huduma ya upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii katika hali ya ukimya na unyenyekevu mkuu. Katika kipindi cha mwaka 2014, barua elfu nane za kuomba msaada kutoka Vatican ziliwasilishwa na kwamba, walisaidiwa, walau kwa kiasi fulani, ingawa si kwa kiwango ambacho kiliombwa. Hii ni huduma inayotolewa ndani na nje ya Italia, kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Jicho la pekee linatolewa kwa Watawa wa ndani ambao wakati mwingine wanakosa mahitaji msingi, kwani wanatumia muda wao mwingi kwa ajili ya sala na tafakari, zinazoliwezesha Kanisa kusonga mbele katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukazia kwamba, maskini wa kiroho na kimwili ni hazina na amana ya Kanisa, ni shule tosha ya unyenyekevu katika hija ya maisha ya mwanadamu, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujifunza pia kutoka kwa maskini ili kugundua siri ya urembo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.