2015-05-12 10:38:00

Siku ya akina Mama: Mwombeni Bikira Maria awasaidie kutekeleza wajibu!


Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Tafakari ya Sala ya Malkia wa Mbingu, Jumapili iliyopita, aliwakumbuka na kuwapongeza akina Mama wote popote pale walipo; wale wanaoendelea kuishi hapa duniani bila kuwasahau wale waliotangulia mbele za haki. Aliwaombea baraka na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ambaye, Kanisa linafanya Ibada ya pekee wakati huu wa Mwezi Mei.

Askofu mkuu GianCarlo Bregantini, Askofu mkuu wa Jimbo kuu Campobasso-Bojano katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Mama Duniani, anasema kwamba, hii ni siku kuu ambayo inamguso wa pekee katika maisha ya watu; kwani akina mama ni kielelezo cha huduma, ukarimu na upendo usiokuwa na mipaka. Kuna wanawake wengi ambao wanaendelea kujisadaka kwa ajili ya kudumisha Injili ya Uhai, kwa kuwapatia watoto nafasi ya kukua, kukomaa na kuishi kadiri ya mapenzi mema, hata kama ukarimu na upendo huu una gharama zake.

Jumuiya ya Kimataifa inapowakumbuka na kuwaenzi wanawake, kwa namna ya pekee, haiwezi kuwasahau wanawake kutoka Barani Afrika ambao wanaendelea kulia kila siku kutokana na watoto wao kufa maji baharini, wakiwa na matumaini ya kupata maisha bora zaidi Barani Ulaya! Lakini kwa bahati mbaya, wanakumbana na kifo na ndoto zao zinafukiwa kwenye tumbo la Bahari ya Mediterrania. Huu ndio ukweli wa maisha yanayowasibu wahamiaji na wakimbizi wengi kutoka Barani Afrika na kwingineko ambako kuna vita, kinzani na migogoro.

Bikira Maria aliyehifadhi yote moyoni mwake, awasaidie wanawake sehemu mbali mbali za dunia wanaoendelea kuomboleza kwa kuondokewa na watoto wao wanaokufa maji Baharini, wanaouwawa kutokana na vita na kinzani mbali mbali. Pamoja na magumu yote, akina mama wawe na ujasiri wa kuwasikiliza, kuwasaidia na kuwahudumia watoto wao kwa upendo mkuu. Dhamana hii iendelezwe pia na walimu na walezi mbali mbali, kwani moyo mpendelevu wa mama unaokoa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.