Jumapili, Papa Francisko akikumbuka kukutana kwake na Papa Tawadros II, wa Kanisa la Kikoptiki la Kiotodosi la Alexandria, miaka miwili iliyopita, kwa moyo wa urafiki na mshikano wa kiroho , alimpigia simu Papa Tawadros II.
Mkurugenzi wa Ofisi ya Habari Vatican , Padre Federico Lombardi, ametaarifu kwamba, mazungumzo ya viongozi hawa wakuu wa Kanisa, kwa njia ya simu , yalilenga hasa katika mada kuu mbili: mapenzi kuendelea katika dhamira yao ya kujenga umoja wa Wakristo na mapendekezo kwa ajili ya kuwa na sherehe moja ya Siku Kuu ya Pasaka.
Papa Francisko katika maelezo yake alimshukuru Mungu kwa umoja na urafiki unaounganisha katika safari ndefu ya urafiki kati ya Jimbo la Papa na Jimbo la Mtakatifu Marko, ambayo ni jumuiya ya Wakristo wa Misri na Mashariki ya kati, Wakristo wanaoendelea kuwa mashahidi jasiri wa Ukristo. Na kwa namna ya kipekee akilitaja kanisa la Kikoptiki ambalo hivi karibuni waamini wake wametoa ushuhuda wa kifodini kwa ajili ya imani yao. Papa amewaombea kafara hao wapokelewe katika ufalme wa Mungu .
Na aliendelea kumshukuru Mungu , kwa hatua zilizokwisha pigwa katika njia ya kutembea pamoja kirafiki , wakiwa wameungana katika kifungo cha ubatizo . Na kwamba hata kama umoja huo haujawa kamili, kuna mambo mengi msingi yanayowaunganisha kuliko yale yanayowatenganisha. Na hivyo akaomba, wadumu katika njia hii hadi kufikia umoja kamili na kukua katika upendo na maelewano.
Katika maelezo yake , Papa kwa namna ya pekee, alionyesha kutiwa nguvu na Tume ya Pamoja ya Kimataifa ya Mazungumzo ya Kiteolojia, kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa ya Mashariki ya Kiotodosi ambayo hivi karibuni imehitimisha rasimu juu ya kazi za Umoja katika Maisha ya Kanisa la Mwanzo na athari zake kwa ajili ya kutafuta ushirika kamili leo hii. Hivyo akaonyesha matumaini yake kwamba, Papa Tawadros II, ataweza kutoa mchango wake katika majadiliano haya muhimu kwa ajili ya kutoa matunda mengi mazuri. Na anafurahi kwamba, Upatriaki wa Jimbo la Mtakatifu Marko, utakuwa mwenyeji wa Mkutano ujao wa Tume hiyo mjini Cairo.
Na alionyesha kujali mahangaiko na mateso ya Wakristo, akisema duniani kote wanakabiliwa na changamoto zinazofanana ambazo zinahitaji kufanya kazi kwa pamoja. Na alipokea kwa mikono miwili uteuzi wa mwaka jana wa wajumbe watakao shiriki kaika Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia, Anatumaini ushirikiano katika suala hili, utaendelea na hasa katika kupata ufumbuzi kwa masuala yanayohusiana na ndoa mseto.
All the contents on this site are copyrighted ©. |