2015-05-11 10:34:00

Mkutano mkuu wa Caritas Internationalis na mapambano ya umaskini na njaa


Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 12 Mei 2015, Jioni saa 11:30 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya maadhimisho ya mkutano mkuu wa XX wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki, Caritas Internationalis.

Ibada hii itatanguliwa na mkutano wa waandishi wa habari, utakaofanywa na viongozi wakuu wa Caritas Internationalis, majira ya asubuhi, kuanzia saa 5: 30 kwenye Ofisi za Habari za Vatican. Kauli mbiu inayoongoza maadhimisho haya ni “Familia moja ya binadamu; utunzaji wa kazi ya uumbaji. Itakumbukwa kwamba, mkutano huu unatarajiwa kuhitimishwa Jumapili tarehe 17 Mei 2015. Zaidi ya wajumbe 300 kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanashiriki, ili kuweka: sera na mikakati ya maendeleo ya kupambana na baa la njaa na umaskini katika kipindi cha miaka minne ijayo.

Baba Mtakatifu Francisko anawachangamotisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwenda pembezoni mwa jamii, ili kuwasaidia watu wanaopambana na umaskini pamoja na baa la njaa kwa kuwatangazia ujumbe wa matumaini na mshikamano wa upendo. Kati ya viongozi wakuu wa Kanisa wanaotarajiwa kuhutubia katika ufunguzi wa mkutano wa Caritas Internationalis hapo tarehe 13 Mei 2015 ni pamoja na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani; Padre Gustavo Gutierrez, OP. mwanataalimungu; Professa Jeffrey Sachs, Dr. Jacques Diouf, mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa Ukanda wa Sahel na Pembe ya Afrika pamoja na Beverly Haddad kutoka Chuo kikuu cha Kwazulu, Natal, Afrika ya Kusini.

Kati ya mambo yanayotarajiwa kujadiliwa anasema Bwana Michael Roy, Katibu mkuu wa Caritas Internationalis ni kuhusu: Usawa, uhamiaji, mabadiliko ya tabianchi, vita na kinzani; kashfa ya njaa na utapiamlo wa kutisha duniani. Hizi ni changamoto ambazo Caritas Internationalis inakabiliana nazo katika kukuza na kudumisha haki na maendeleo endelevu. Itakuwa ni fursa pia ya kuangalia changamoto zitakazotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake kuhusiana na mazingira, kama sehemu ya mchango wa Kanisa katika mkutano wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika mjini Paris, Ufaransa, Desemba 2015.

Kardinali Rodrigues Maradiaga anamaliza kipindi chake kama Rais wa Caritas Internationalis na kwamba, katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika hapo tarehe 14 Mei 2015: wanaogombea nafasi hii  kwa sasa ni Kardinali Luis Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila, Ufilippini pamoja na Askofu mkuu Youssef Soueif, Rais wa Caritas nchini Cyprus. Baada ya maadhimisho ya mkutano mkuu, wajumbe wa mkutano watakwenda Milano kutembelea Onesho la Chakula kimataifa, Milano Expo 2015 kama sehemu ya kampeni ya kupambana na kashfa ya njaa duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.