2015-05-11 10:09:00

Miaka 70 tangu kusitishwa kwa Vita kuu ya Pili ya Dunia: Maafa makubwa


Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 70 tangu Vita kuu ya pili ya Dunia ilipositishwa Barani Ulaya; watu wengi wengi wasiokuwa na hatia walipoteza maisha na kwamba, dunia ilishuhudia maafa makubwa kwa watu na mali zao. Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, matukio kama haya hayajirudii tena.

Kuna watu walipoteza maisha kutokana na imani na ubinadamu wao, watu wengi waliathirika, lakini vijana waliathirika zaidi. Kipindi hiki pia kilionesha mshikamano wa kimataifa dhidi ya utawala wa mabavu na ubaya uliokuwa unatendwa na binadamu. Umoja wa Mataifa unafanya kumbu kumbu ya miaka 70 tangu Vita kuu ya Pili ya Dunia ilipositishwa kwa heshima kubwa kwani huu ulikuwa ni mwanzo wa Umoja wa Mataifa, Jukwaa la kutatua na kusuluhisha matatizo na changamoto za Jumuiya ya Kimataifa katika misingi ya haki na amani, ili kudumisha amani na usalama.

Haya yamesemwa na Bwana Ban Ki-Moon, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati alipokuwa anahutubia kwenye maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 70 tangu Vita kuu ya Pili ya Dunia ilipositishwa Ulaya, kumbu kumbu hii imefanyika nchini Poland. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema kwamba, Jumuiya ya Kimataifa haina budu kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, vijana wa kizazi kipya hawashuhudii tena majanga ya vita, kwani vita imerekebisha dhamana na dira katika kazi ya Umoja wa Mataifa.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, inavalia njuga utekelezaji wa kanuni msingi zinazoojikita katika: amani, utulivu pamoja na kuheshimu haki msingi za binadamu. Maadhimisho haya ni changamoto endelevu ya kihakikisha kwamba, kanuni hizi zinadumishwa na kuendelezwa, ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo.

Kuna haja ya kujenga na kuendeleza majadiliano, ushirikiano wa kimataifa pamoja na kujikita katika sera za maendeleo endelevu, utunzaji bora wa mazingira, haki msingi za binadamu pamoja na kukomesha kinzani na misigano. Jumuiya ya Kimataifa haina budu kudumisha misingi ya demokrasia hususan katika nchi ambazo bado ziko katika kipindi cha mpito. Vita na kinzani bado ni changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo, hivyo Jumuiya ya Kimataifa iwe makini katika kudumisha amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.