2015-05-11 10:25:00

Maisha ya ndoa na familia: Wekeni uwiano sawia kati ya kazi na familia


Baraza la Maaskofu Katoliki Canada kuanzia tarehe 11 hadi tarehe 17 Mei 2015 linaadhimisha Juma la Kitaifa la familia linaloongozwa na kauli mbiu “Maridhiano kati ya Familia na Kazi”. Maaskofu Katoliki katika barua yao ya kichungaji kwa ajili ya maadhimisho haya wanakazia umuhimu wa kuthamini, kukuza na kuendeleza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwa kutambua mchango wake katika ustawi na maendeleo ya jamii ya wananchi wa Canada.

Maaskofu wanasema, familia ni shule ya maisha, mahali ambapo mwanadamu tangu mwanzo anajifunza kujisadaka kwa ajili ya ndugu zake; ni mahali pa mtu kujifunza kuonja na kuwagawia wengine upendo, huruma na msamaha unaobubujika kutoka katika undani wa mwanadamu. Lakini kutokana na utandawazi, maendeleo ya sayansi na teknlojia, leo hii familia nyingi zinakumbana na matatizo na changamoto nyingi, kumbe kuna haja kwa familia kuhakikisha kwamba, zinatekeleza wajibu wake wa kitaaluma, bila kusahau majukumu ya kifamilia.

Changamoto hii ni kubwa kwa wanawake ambao wanafanya kazi katika mazingira magumu, kiasi kwamba, kwa upande wao, familia inapewa uzito kidogo, ikilinganishwa na fursa za kazi zilizopo, kwani hawana njia mbadala, bali wanalazimika kutenda kadiri ya mazingira. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, familia ina dhamana na wajibu wa kutoa huduma makini kwa wanajumuiya wake: kwa kuhakikisha kwamba, wanapata malezi na makuzi; zawadi ya maisha inalindwa na kudumishwa; sanjari na kusimamia haki msingi za kifamilia.

Maaskofu wanasema, maridhiano kati ya familia na kazi si tatizo la mtu binafsi, bali ni changamoto kubwa inayopaswa kufanyiwa kazi na Familia ya Mungu nchini Canada, inayopaswa kuhakikisha kwamba, inawasaidia watu binafsi kutekeleza dhamana na majukumu yao katika familia. Hii inatokana na ukweli kwamba, watoto ndani ya familia wanahitaji malezi na makuzi ya wazazi na walezi wao. Vijana na wazee wanahitaji pia kuonjeshwa mshikamano wa dhati.

Kuna wakati mwingine, wanawake wanaamua kuacha kazi kwa ajili ya kuhudumia familia zao, jambo ambalo linaonesha ujasiri wa pekee kabisa, lakini jamii inapaswa kujenga mazingira yatakayowawezesha wanawake kufanya kazi sanjari na kutekeleza wajibu wao wa kifamilia bila kulazimika kuacha kazi, kwani kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada katika maadhimisho ya Juma la Familia Kitaifa, linapenda kuwahimizwa wanasiasa na watunga sera kutambua umuhimu wa familia katika ustawi na maendeleo ya jamii ya watu na kwamba, kuna haja ya kujenga mahusiano mema kati ya kazi na wajibu wa familia, ili kweli familia ziweze kutekeza dhamana yake barabara pamoja na kuendelea kuchangia katika ustawi na maendeleo ya jamii nzima ya watu wa Canada. Yesu Kristo anawaunga mkono wale wote wanaojibidisha ili kuhakikisha kwamba, wanajenga mazingira bora kwa maisha ya familia nchini Canada na kwamba, Roho Mtakatifu anaendelea kusaidia mchakato wa maboresho ya tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, kumbe hapa kuna haja kwa Familia ya Mungu nchini Canada kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili kweli aweze kuwafunda, tayari kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya Familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.