2015-05-09 17:22:00

Sikilizeni kilio cha mateso na mahangaiko ya watu duniani!


Mkutano wa kwanza kimataifa kati ya Marabbi, Makardinali na Maaskofu uliokuwa umeandaliwa na Chama cha Ukatekumene mpya kwa kusimamiwa na Kiko Arguello umhitimishwa hivi karibuni huko Galilaya, nchini Israeli, kama kumbu kumbu ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Waraka kuhusu Majadiliano ya kidini, Nostra Aetate sanjari na kumbu kumbu ya miaka 70 tangu kuhitimishwa kwa Shoah, yaani mauaji ya kinyama dhidi ya Wayahudi. Mkutano huu umehudhuriwa pia na watu mashuhuri kutoka katika ulimwengu wa wasomi, sanaa na tamaduni kutoka katika dini ya Kikristo na Kiyahudi.

Mkutano huu wa aina yake ni matokeo ya hamasa iliyotolewa na Vatican katika kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini mbali mbali ili kujenga umoja, udugu na urafiki kati ya waamini wa dini hizi mbili. Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua umuhimu wa tukio hili, amewaandikia washiriki ujumbe wa matashi mema, kwa kuonesha uwepo wake wa karibu: kiroho. Anasema, hii ni fursa ya kukuza na kudumisha mshikamano wa upendo, ili kusikiliza kwa makini kilio cha damu ya watu wasiokuwa na hatia kwa njia ya lugha ya muziki.

Baba Mtakatifu anasema, anapenda kuungana nao, ili kusali na kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kusikiliza kilio cha damu ya watu wasiokuwa na hatia, ili hatimaye, aweze kuponya madonda ya wale ambao wanateseka kutokana na madhulumu haya. Ni sala ya Baba Mtakatifu kwamba, watu wataweza pia kufungua mioyo yao, ili kusikiliza kilio cha damu ya watu wasiokuwa na hatia kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kweli amani iweze kutawala katika mioyo ya watu.

Katika mkutano huu, viongozi hawa wa kidini wamejadili na kugusia changamoto wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa dhamana ya wokovu miongoni mwa Wayahudi na Wakristo katika ulimwengu mamboleo; urithishaji wa imani kwa vijana wa kizazi kipya; kuibuka kwa kasi kwa wamini wenye misimamo mikali ya kiimani. Kwa pamoja viongozi hawa wa kidini wanakiri kwamba, tukio hili la kihistoria limewawezesha kukutana na Marabbi wengi kiasi hiki na kwamba, wanapongeza juhudi zinazofanywa na Chama cha Kitume cha Ukatekumeni mpya katika mchakato wa kueneza imani sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.