2015-05-09 18:09:00

Rozari takatifu ni Biblia ya waamini wa kawaida! Muhtasari wa Injili


Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Wakleri, tarehe 8 Mei 2015 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea amani duniani kutoka kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu wa Pompei, Italia. Katika mahubiri yake, Kardinali Stella amekazia umuhimu wa toba na wongofu wa ndani kama sehemu ya mchakato wa kuchuchumilia utakatifu wa maisha pamoja na kuendelea kujibidisha kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Yesu katika maisha. Anasema, Ibada ya Rozari takatifu ni muhtasari wa Injili, unaowasaidia waamini kwa njia ya Bikira Maria, kumfahamu zaidi Yesu Kristo, Mkombozi wa dunia.

Kardinali Stella anawahimiza waamini kuhakikisha kwamba, wanashuhudia imani yao kwa njia ya matendo ya huruma ambayo wanapaswa kuwaonjesha binadamu wa leo wanaokabiliwa na magumu pamoja na changamoto mbali mbali za maisha. Hawa ni wakimbizi na wahamiaji wanaokimbia vita na majanga mbali mbali ya maisha. Ni binadamu wenye utu na heshima zao, wanapaswa kuthaminiwa hata katika umaskini wao.

Askofu mkuu Tomaso Caputo katika salam zake ameelezea jinsi ambavyo Pompei ilivyoshiriki kuwapokea na kuwakirimia wahamiaji na wakimbizi waliokolewa hivi karibuni kutoka kwenye Bahari ya Mediterrania, watu ambao wamepambana uso kwa uso na kifo! Maelfu ya waamini wameshiriki katika Ibada ya Rozari kwa Bikira Maria wa Pompei, iliyoanzishwa kunako mwaka 1883 na Mwenyeheri Bartolo Longo, mwaliko kwa waamini kutubu na kumwongokea na kuambatana na Mwenyezi Mungu. Mwelekeo huu uwasaidie waamini kujiandaa vyema kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Kardinali Stella anawataka waamini kujibidisha kumfahamu Yesu Kristo, tayari kumjibu kwa njia ya upendo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha, kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji. Hata katika umaskini, mapumngufu yao ya kibinadamu na dhambi zinazowaandama kila siku, lakini wana kitu ambacho wanaweza kukitoa kwa ajili ya mafao ya wengine.

Watambue kwamba, wamekombolewa kwa njia ya Damu Azizi ya Yesu Kristo, kumbe wana thamani kubwa machoni pa  Mungu. Rozari takatifu ni Biblia kwa watu wa kawaida, mahali ambapo waamini wanaweza kumfahamu Yesu kwa njia ya Bikira Maria. Kusali Rozari ni kufanya tafakari ya kina kuhusu Mafumbo ya maisha na utume wa Yesu, kwa kutumia akili ya imani na unyenyekevu wa moyo.

Waamini wa Pompei, wanaendelea bado kukumbuka hija ya kitume iliyofanywa na Baba Mtakatifu Francisko Madhabahuni hapo, tarehe 21 Machi 2015, ilikuwa ni fupi, lakini imeacha chapa ya kudumu katika maisha ya waamini na watu wenye mapenzi mema, hasa kwa kujikita katika huduma ya upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hapa ni mahali ambapo waamini wanakwenda kuomba msamaha wa dhambi ili kuonja huruma ya Mungu. Kardinali Beniamino Stella mara baada ya Misa Takatifu ametembelea na kushuhudia kazi mbali mbali zinazotekelezwa Pompei kama kielelezo cha matendo ya huruma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.