2015-05-09 16:58:00

Msumbiji: Jengeni utamaduni wa kukutana, kushirikiana na kutetea uhai!


Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji halina budi kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana, kushirikiana na kusimama kidete ili kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya Familia na Uhai. Ni mwaliko kwa Kanisa kujielekeza zaidi katika kutoa huduma ya upendo kwa wakimbizi na wahamiaji, ili waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi, tarehe 9 Mei 2015 wakati alipokutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji, wakati huu linapofanya hija ya kitume mjini Vatican. Baba Mtakatifu anapenda kushiriki furaha, matumaini na mahangaiko ya wananchi wa Msumbiji na kwamba, anawashukuru Maaskofu kwa huduma makini wanayoifanya kwa ajili ya kuwahudumiwa Watu wa Mungu majimboni mwao na kwamba, yuko pamoja nao katika hija hii ya maisha ya kiroho.

Baba Mtakatifu anawakumbusha Maaskofu kwamba, wanapaswa kumuiga Yesu Kristo mchungaji mwema, aliyejisadaka kwa ajili ya Kondoo wake, mwaliko kwa Maaskofu pia kuwa viongozi wanaojipambanua kwa njia ya unyenyekevu unaojionesha katika huduma makini. Watoe kipaumbele cha pekee kwa Mapadre ambao ni wasaidizi wao wakuu katika mchakato wa Uinjilishaji wa watu; wawasaidie na kuwahudumia kama wazazi, ndugu na rafiki pamoja na kuhakikisha kwamba wanapata muda wa kukaa na kuzungumza na Mapadre wao. Moja ya majukumu makuu ya Askofu ni kuhakikisha ustawi na maendeleo ya Mapadre wake, hususan nyakati za shida na magumu wanapotekeleza dhamana na utume wao kwa Familia ya Mungu.

Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwashukuru Wamissionari ambao wanaendelea kukumbatia Msalaba wa Kristo, kwa ajili ya kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu. Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, iwe ni fursa ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ajili ya ushuhuda na huduma inayotolewa na watawa wa mashirika mbali mbali nchini Msumbiji. Ni watu ambao wanaendelea kujisadaka kwa maskini na huduma kwa Familia ya Mungu katika medani mbali mbali za maisha: kiroho, kimwili, kimaadili na kiutu.

Baba Mtakatifu anasema watawa ni watu ambao wanapeta katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii, changamoto ni kuhakikisha kwamba, Majimbo yanajitahidi kutumia vyema karama za Mashirika haya ya kitawa ili kuyatajirisha Majimbo na kamwe wasiwe ni ”viraka” vya kuziba mapengo Majimboni. Kuwepo na sera na mikakati makini, inayotekelezwa kwa pamoja, kwani Maaskofu wana dhamana ya kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa Familia ya Mungu majimboni mwao.

Maaskofu wasaidie kutoa matumaini kwa wale waliokata tamaa, wale waamini wanaoonesha hamu ya kutaka kurejea tena nyumbani, katika familia au Kanisani Maaskofu waendele kushirikiana na kushikamana kama Kanisa mahalia na Kanisa la kiulimwengu, ili kujenga na kudumisha Kanisa kama Familia ya Mungu inayowajibika. Wajenge na kuendeleza majadiliano kwa kushirikiana na Mabaraza ya Wakleri, Halmashauri Walei na Baraza la Uchumi; mambo msingi katika utekelezaji wa shughuli za kichungaji Majimboni.

Wananchi wa Msumbiji wajitahidi kujenga na kuendeleza utamaduni wa watu kukutana, ili kusaidia waathirika wa majanga asilia; kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na upatanisho wa kitaifa. Hii inatokana na ukweli kwamba, vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Msumbiji ilisababisha utengano wa kitaifa na misigano ya kijamii.

Vijana wafundwe tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili, tayari kuchangia katika ustawi na maendeleo ya nchi yao. Kanisa liendelee kuimarisha mahusiano mema na Serikali kwa ajili ya mafao ya wengi, hasa kwa ajili ya kulinda na kutetea familia na Injili ya Uhai, tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Maaskofu wasiwe na wasi wasi ya kuachwa pweke, kwani Yesu mwenyewe amewahakikishia kwamba, atakuwa pamoja nao hadi utimilifu wa dahali. Maaskofu waoneshe ujasiri wa kumfuasa Kristo ili kuwatangazia Watu wa Mataifa, Habari Njema ya Wokovu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.