2015-05-08 08:24:00

Siri ya Watoto wa Fatima: Hapa hakuna mzaha, waamini wawe makini!


Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema kwamba, Kanisa katika ulimwengu mamboleo ni Kanisa la mashuhuda ambalo linaendelea kujengwa kutokana na damu ya watoto wake inayomwagika sehemu mbali mbali za dunia. Kuna watu wanauwawa, wanayanyaswa na kudhulumiwa kutokana na chuki za kidini. Huu ndio ukweli uliokuwa umefumbatwa katika ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima, yaani Francis. Lucia na Yacinta. Ni Siri inayogusa matukio ya kihistoria, maisha na utume wa Kanisa.

Hata leo hii, Kanisa linaendelea kujaribiwa, kwa baadhi ya watu kutaka kujenga hisia za chuki na uhasama dhidi ya Kanisa pamoja na kupandikiza mbegu ya kifo. Bikira Maria alipowatokea watoto wa Fatima, aliwapatia Siri kuu tatu ambazo zote zimekwisha fafanuliwa na viongozi wa Kanisa kwa wakati wake. Ni siri ambazo zimejikita katika mwono wa vita, majanga, kinzani na migawanyiko kati ya watu. Siri zote hizi ziliandikwa na Sr. Lucia. Siri ya tatu hakikuweza kufunuliwa kutokana na amri iliyotolewa na Askofu mahalia.

Papa Yohane Paulo II baada ya jaribio la kutaka kumuua kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro hapo tarehe 13 Mei 1981 aliamuru kwamba, siri ya tatu ifunuliwe na kuwekwa hadharani. Tafsiri ya siri hii ilitolewa na Kardinali Joseph Ratzinger, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la mafundisho tanzu ya Kanisa, alisema kwamba, siri ya tatu ya Fatima ilikuwa ni mwaliko kwa Wakristo kusoma alama za nyakati na kutoa majibu muafaka kwa njia ya ushuhuda wa imani.

Mtakatifu Yohane Paulo II anakiri kwamba, ni mkono na kinga ya Bikira Maria iliyomwezesha kusalimika katika jaribio la kutaka kumuua hapo tarehe 13 Mei 1981. Sala ni nguzo muhimu sana katika maisha dhidi ya wasi wasi wa kifo anasema Mtakatifu Yohane Paulo II. Huu ni ufafanuzi ambao umetolewa na Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu wakati alipokuwa anatoa mhadhara kwenye Chuo kikuu cha Kipapa cha Antonianum kuhusu ujumbe wa Fatima kati ya Karama na Unabii.

Kuanzia tarehe 7 Mei hadi tarehe 30 Septemba 2015, Sanamu ya Bikira Maria wa Fatima inatembezwa kwenye baadhi ya majimbo ya Kanisa Katoliki nchini Italia, kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani na maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia. Hiki ni kipindi kwa ajili ya kuombea amani, miito mitakatifu, upendo na mshikamano kati ya wanandoa.

Kardinali Angelo Amato anasema kuhusu mwono wa Siri ya Fatima, ni changamoto ya kuangalia kinzani zinazojitokeza ili kuona na hatimaye kutenda, kwa msaada wa maombezi ya Bikira Maria, ili kupata jibu makini katika mwanga wa imani; kwa kuwa makini pamoja na kusimama kidete kupambana na Shetani anayejionesha kwa sura mbali mbali katika maisha ya mwanadamu.

Sr. Lucia anawaonesha waamini mambo msingi ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wao: kujikita katika kutenda mema, kuwa mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo; kwa kumwabudu na kumtukuza Mungu, chemchemi ya imani, matumaini na mapendo. Waamini wajenge utamaduni wa kusali Rozari takatifu, kwani huu ni muhtasari wa Injili pamoja na kuendeleza Ibada kwa Moyo Safi wa Bikira Maria sanjari na kukomalia utakatifu wa maisha ya familia.

Kardinali Angelo Amato anasema kwamba, Sr. Lucia pamoja na mambo mengine, alikazia mambo makuu mawili: msamaha na utakatifu wa maisha; kwa kumwomba Mwenyezi Mungu msamaha wa dhambi zinazotendwa ulimwenguni na watu mbali mbali. Msamaha ni zawadi inayohitaji sadaka na majitoleo endelevu, mwaliko wa kujikita katika fadhila ya upendo pasi na kukata tamaa.

Mwaliko wa pili unawaelekeza zaidi watawa, kwani hawa wanachangamotishwa na Bikira Maria kuwa kweli ni watakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Wajitahidi kukita maisha yao katika toba na wongofu wa ndani; sala na matendo ya huruma kiroho na kimwili. Watawa wawe makini ili wasimezwe na malimwengu, bali daima wawe makini kuambatana na neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.Fatima ni ujumbe wa matumaini kwa furaha ya uzima wa milele.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.