2015-05-08 10:38:00

Kanisa linakazia: Michezo, Elimu na Kazi kwa ajili ya majiundo ya mtu!


Michezo, elimu na kazi ni mambo muhimu sana katika majiundo ya mtu mzima, kwani vijana na watoto wanaanza kupata malezi msingi kutoka katika familia na hatimaye kuendelezwa wanapokuwa shuleni. Mambo haya yanapokamilishana, hapo mwanadamu ana uhakika wa kupata utimilifu wa maisha yake na hivyo kuondokana na mambo ambayo yanaweza kuhatarisha ustawi na maisha yake kwa siku za usoni.

Mama Kanisa anatoa kipaumbele cha pekee kwa michezo kwani anatambua kwamba, michezo ni sehemu muhimu sana katkka makuzi ya binadamu, mahusiano na tasaufi ya maisha. Viongozi, wanamichezo na mashabiki wanapaswa kuwa ni mashuhuda wazuri wa tunu msingi za maisha ya binadamu; walezi bora katika mwanga na ukweli. Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 8 Mei 2015 wakati alipokutana na kuzungumza na Shirikisho la Mpira wa Tennis nchini Italia.

Baba Mtakatifu anasema mpi wa wa Tennis una ushindani mkubwa, lakini ili kupata matokeo mazuri hakuna sababu ya kutumia dawa za kuongeza nguvu, hali ambayo inaweza kumpatia ushindi kwa kukiuka sheria na kanuni pamoja na kuwadanganya wengine. Mtakatifu Paulo anasema kwamba, washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja. Huu ni mwaliko wa kupiga mbio ili wao pia waweze kupata tuzo hii, mang’amuzi ya kila siku katika mpira wa Tennis.

Baba Mtakatifu anawataka wadau mbali mbali wa michezo kushindana katika maisha, kwa kutafuta kilicho chema na kizuri bila woga, kwa ari na ujasiri mkuu, kwa kushirikiana na wengine pamoja na Mwenyezi Mungu, daima wakijitahidi kutoa kilicho bora katika maisha yao. Ni mwaliko kwa wanamichezo kutumia karama zao kwa ajili ya ujenzi wa mchakato wa madaraja ya watu kukutana katika urafiki kwa kuwakumbatia wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.