2015-05-07 08:29:00

WCC: Tarehe 10 Mei 2015 ni Siku ya kuombea amani Sudan ya Kusini


Baraza la Makanisa Ulimwenguni, Jumapili tarehe 10 Mei 2015 limeitisha siku maalum yak usali na kufunga kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wananchi wa Sudan ya Kusini ambao wanaendelea kuteseka kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe inayojikita katika uchu wa madaraka, badala ya kusimamia mafao na maendeleo ya wengi.

Lengo la siku hii ya sala ni kumlilia Mwenyezi Mungu ili asaidie kulainisha mioyo ya viongozi wa kisiasa, ili waweze kuanza mchakato wa majadiliano ya kisiasa kama sehemu ya ujenzi wa misingi ya haki, amani, maridhiano, upatanisho na umoja wa kitaifa. Dr. Olav Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anakumbusha kwamba, vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan ambayo imedumu kwa takribani miezi 17 imesababisha maafa makubwa kwa wananchi wa Sudan ya Kusini.

Wananchi wanasubiri kwa hamu na matumaini kuona tena amani, ustawi na maendeleo vikipewa kipaumbele cha pekee katika sera na mikakati ya wanasiasa, ambao kwa sasa wanaonekana kuelemewa zaidi na uchu wa madaraka, wakati wananchi wanaendelea kuteseka na kufa kutoka na vita. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linayaalika Makanisa wanachama kutenga Jumapili ijayo kwa ajili ya kuombea amani, msamaha na upatanisho Sudan ya Kusini.

Baraza la Makanisa Sudan ya Kusini linabaianisha kwamba, hakuna sababu msingi wala ya kimaadili inayoweza kuhalalisha vita inayoendelea huko Sudan ya Kusini. Wanasiasa wanapaswa kuguswa na mahangaiko ya wananchi, tayari kuanza mchakato wa majadiliano ya kisiasa katika ukweli, uwazi na mafao ya wengi nchini Sudan ya Kusini. Wananchi wamechoka kusikia mtutu wa bunduki kila siku ya maisha, mambo yanayokwamisha ustawi na maendeleo ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.