2015-05-07 07:50:00

Ulinzi kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro: Ni wito na dhamana nyeti!


Kikosi cha walinzi wa Papa kutoka Uswiss, maarufu kama “Swiss guards” kina dhamana na utume unaojikita katika wito, uaminifu, umakini na sadaka inayotekelezwa kwa moyo wa unyenyekevu. Huu ni wosia ambao Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amewapatia wanajeshi wapya wa Kikosi cha ulinzi wa Papa kutoka Uswiss waliokula kiapo cha utii na uaminifu kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Jumatano tarehe 6 Mei 2015, Siku ambayo wanawakumbuka askari 147 kutoka Uswiss walioyamimina maisha yao mjini Roma kwa ajili ya kumtetea Khalifa wa Mtakatifu Petro kunako mwaka 1527.

Kardinali Parolin katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya wanajeshi hawa ambao, baadaye jioni walikula kiapo cha utii na uaminifu, amewakumbusha kwamba, hii ni siku maalum ya kukumbukwa katika maisha yao, wanapojitosa kimasomaso kwa ajili ya ulinzi kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Siku ya shukrani sanjari na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, ili yeye aliyeanzisha kazi hii njema ndani mwao, aweze kuikamilisha kadiri ya mapenzi yake.

Kardinali Parolin anawataka wanajeshi hawa kuungana na kudumisha maisha yao na Kristo, ili waweze kuzaa matunda yanayokusudiwa yaani: toba, wongofu wa ndani na maisha ya sadaka yanayowang’oa kutoka katika ubinafsi; tayari kupambana na mapungufu yao ya kibinadamu; daima wakitafuta mafao ya wengi na kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo. Wanapaswa kushikamana na Yesu, ili kuendelea kufurahia maisha, nje ya Yesu watanyauka na kupotelea gizani.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Angelo Becciu, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican katika hotuba yake kwa ajili ya kuwakumbuka askari 147 kutoka Uswiss waliojisadaka kwa ajili ya ulinzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, amewapongeza kwa kuonesha ujasiri na sadaka, kwa ajili ya Mungu na jirani zao. Hii ni siku kuu ya kumbu kumbu, shukrani na matumaini kwa siku za usoni. Baba Mtakatifu pamoja na wasaidizi wake wote, wanawashukuru wanajeshi hawa na wanatambua mchango na dhamana yao katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.  Nishani walizopewa baadhi ya wanajeshi ambao wameonesha ujasiri wa pekee, kiwe ni kichocheo cha moyo wa huduma kwa askari vijana.

Kamanda Christoph Graf  katika hotuba yake, amewakumbuka maelfu ya watu wanaoendelea kufariki dunia sehemu mbali mbali za dunia kutokana na vita, majanga ya maisha, ubaguzi, nyanyaso na dhuluma za kidini, kama hali inavyojionesha huko Iraq na Syria. Tukio hili limehudhuriwa na viongozi na wageni mbali mbali kutoka ndani na nje ya Vatican. Inapendeza kuona jinsi Askari hawa wenye mavazi yanayopendeza, wakitembea kwa mwendo wa kunyata, utadhani Twiga, kwa ukakamavu kana kwamba, Simba yuko mawindoni, lakini wanyenyekevu utadhani ni njiwa! Yaani hadi raha wanasema Waswahili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.