2015-05-07 11:29:00

Mwanadamu kwa asili ni mwanamichezo! Dumisheni pia maisha ya kiroho!


Chama cha Michezo Mkoa wa Lazio, Italia kinaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 115 tangu kilipoanzishwa na kundi la vijana, waliokuwa wanataka kuwarithisha vijana wenzao tunu msingi za maisha ya kimaadili na kimichezo. Hii ni changamoto endelevu kwa wanamichezo kuwa wakarimu na kuthamini karama mbali mbali ambazo wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu, ili kujenga na kudumisha udugu na utulivu kati ya watu.

Katika amani mambo madogo madogo hukua na kuongezeka katika utengano mambo makuu yanaanguka na kupotea. Katika kipindi cha miaka yote hii, Lazio imejipambanua kwa kucharuka katika masuala ya michezo, kwa kuwa na wadau, wanamichezo na mashabiki, ambao wanaungana kwa pamoja ili kushuhudia mshikamano kwa kuonesha usawa katika masuala ya michezo, jambo ambalo Lazio imelivalia njuga kwa miaka mingi. Mpira wa miguu unaonekana kupewa kipaumbele cha pekee katika michezo, kiasi hata cha kupuuzia michezo mingine.

Hii ni hotuba ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Chama cha Michezo cha Mkoa wa Lazio, Italia, walipomtembelea mjini Vatican, tarehe 7 Mei 2015. Ikumbukwe kwamba, kila mchezo una thamani yake: kimaadili na kijamii kwani inawasaidia vijana kukua katika uwiano sawia, kwa kujizuia, kwa kuonesha moyo wa sadaka pamoja na kuwajali wengine.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, binadamu kwa asili ni mwanamichezo, changamoto ya kukuza na kudumisha mwelekeo wa maisha ya kiroho hata katika masuala ya michezo. Vijana wahamasishwe kushiriki kikamilifu katika Ibada ya Misa Takatifu na Katekesi kwani haya pia ni mambo muhimu katika majiundo ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Vijana wafundwe kuthamini masomo, urafiki na huduma kwa maskini.

Kuna wanamichezo mashuhuda wa imani na huduma ambao wamekuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa jamii inayowazunguka. Kwa njia ya michezo, Jamii inaweza kujenga moyo wa udugu na mshikamano na hivyo kuondokana na mambo yanayosababisha ukosefu wa haki na majanga katika maisha ya watu na jamii katika ujumla wake. Chama cha michezo cha Lazio, hakina budi kuwa ni chombo cha huduma ya mshikamano kati ya vijana na familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.